Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ameitumia salamu za rambirambi familia ya mmoja wa Waasisi wa Taifa la
Tanzania Ndg. Paul Sozigwa aliyefariki dunia jana tarehe 12 Mei, 2017
Jijini Dar es Salaam.
Katika
Salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amesema Marehemu Paul Sozigwa
atakumbukwa kwa utumishi wake uliotukuka kwa Taifa, uchapakazi na
uadilifu.
“Natambua
kuwa Marehemu Paul Sozigwa ni miongoni mwa Waasisi wa Taifa letu ambao
walijitoa kwa dhati kuipigania nchi yetu kabla na baada ya uhuru,
alishirikiana na Waasisi wengine wa Taifa letu akiwemo Baba wa Taifa
Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, kukabiliana na changamoto
mbalimbali zilizolikabili Taifa letu baada ya uhuru zikiwemo kupiga vita
umasikini, ujinga na maradhi ndani ya Chama na Serikali, hakika
tutazienzi juhudi zake” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameitumia salamu za rambirambi familia ya
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ndg. Said Mwambungu aliyefariki dunia
jana tarehe 12 Mei, 2017 katika hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar
es Salaam.
Mhe.
Rais Magufuli amesema Marehemu Saidi Mwambungu atakumbukwa kwa
uchapakazi wake, busara, uongozi mahiri, na uzalendo wake kwa Taifa
alipokuwa kiongozi ndani ya Serikali na katika Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
“Ndg.
Said Mwambungu alikuwa ni kiongozi wa aina yake, moyo wake wa upendo
ulimwezesha kufanikiwa katika kazi zake nyingi, siku zote alipigania
maendeleo ya wananchi na hakushindwa kutatua jambo kwa njia ya
mazungumzo, hakika tutaukumbuka na kuuenzi mchango wake” amefafanua Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli amewapa pole nyingi wanafamilia, wanachama wa CCM, na
wananchi wote walioguswa na vifo hivyo na amewaombea wapumzike mahali
pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam