Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewatia hatiani, Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania ya Viettel inayofanya
biashara kama Halotel, Do Hong na wenzake wanane, kwa kosa la kuhujumu
uchumi na kuwataka kulipa faini ya zaidi ya Sh. milioni 700.
Hata
hivyo, Hong ameachiwa huru baada ya kulipa Sh milioni 479 ambazo kati
yake, sh milioni 20 ni faini na sh milioni 459 ni fidia ya hasara
anayodaiwa kuitia Serikali.
Wenzake
wamekwenda jela kwa kutolipa. Mbali ya Hong, washitakiwa wengine ni
Dilshad Ahmed (36), Rohail Yaqoob (47), Khalid Mahmood (59), Ashfaq
Ahmad (38), Muhamad Aneess (48), Imtiaz Ammar (33) wote raia wa
Pakistan, Ramesh Kandasamy (36) raia wa Sri-Lanka na Viettel Tanzania
Limited (Halotel) iliyoshitakiwa pia.
Hakimu
Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Wilbard Mashauri alitoa hukumu hiyo
jana baada ya washitakiwa hao kukiri makosa yao baada ya kusomewa upya
mashitaka saba badala ya 10 waliyokuwa wameshitakiwa nayo kwa maelezo ya
awali.
Mashitaka
waliyoshitakiwa nayo katika kesi hiyo ni kula njama kutenda kosa,
kughushi na kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa. Hakimu Mashauri alisema
katika kila kosa mshitakiwa atatakiwa kulipa Sh milioni tano na
wanatakiwa kurudisha hasara yote walioisababishia serikali, ya Sh
milioni 459.
“Washitakiwa
hawa wamekuja kuwekeza nchini na lengo sio kuhujumu uchumi na
miundombinu yetu. Ili iwe fundisho kwa wawekezaji wengine na kuonesha
kwamba Tanzania ipo makini katika masuala haya, kila mshitakiwa
atatakiwa kulipa Sh milioni tano na kuilipa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) fedha walizohujumu,” alisema Hakimu Mashauri katika hukumu.
Pia
Hakimu huyo aliagiza vifaa vyote walivyokutwa navyo washitakiwa
wakifanyia biashara, vitaifishwe na serikali na akasema wanayo haki ya
kukata rufaa Mahakama Kuu kuhusiana na adhabu pekee.
Kabla
ya kutolewa kwa adhabu, Wakili wa Serikali, Jehovaness Zacharia, alidai
hawana kumbukumbu ya makosa ya zamani ya washitakiwa hivyo mahakama
iwape adhabu inayostahili kulingana na makosa.
Katika
mashitaka yao, inadaiwa kuwa kati ya Novemba 2016 na Februari 2017,
Jijini Dar es Salaam, walitengenezamfumo wa kutumia huduma za mtandao
kwa lengo la kukwepa kodi ya kupokea na kusambaza simu za kimataifa bila
kibali cha TCRA. Pia wanadaiwa katika kipindi hicho waliendesha hiyo
mifumo ya kupokea na kusambaza simu za kimataifa bila ya leseni.
Inadaiwa
Novemba 20, 2016 waliingiza vifaa vya kielektroniki bila ya kuwa na
leseni ambapo katika tarehe isiyofahamika Novemba 2016, walisimika vifaa
hivyo ikiwamo sim box yenye namba ya siri 1152000.8.n.t.n na Laptop
mbili aina ya Dell bila ya kuwa na kibali cha TCRA.
Katika
kipindi hicho, washtakiwa hao wanadaiwa kuunganisha vifaa hivyo na
huduma za mitandao kwa lengo la kupokea na kusambaza mawasiliano bila ya
kuthibitishwa na TCRA itakavyo sheria.
Viettel
Tanzania Limited (Halotel) na Do Hong, wanadaiwa kati ya Novemba 2016
na Februari 2017 maeneo ya ofisi za Halotel Victoria Kinondoni,
walishindwa kuthibitisha taarifa iliyotolewa na Unex Company Ltd
kusajili laini za simu 1,000. Pia inadaiwa washtakiwa hao kwa pamoja
wanadaiwa kuisababishia hasara TCRA na serikali ya Tanzania ya Sh
459,000,000.
0 comments:
Chapisha Maoni