Siku
moja baada ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Bungu
wilayani Kibiti, Alife Mtulia, kuuawa kwa kupigwa risasi na watu
wasiojulikana akiwa nyumbani kwake, imeelezwa kuwa wauaji hao waliacha
ujumbe wakidai marehemu alikuwa akidhulumu watu.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema mauaji hayo yalifanyika
usiku wa kuamkia jana, huku akiahidi kutoa ufafanuzi wa kina leo.
Mauaji
ya askari Polisi, viongozi wa Serikali za Mitaa na raia yamekuwa
yakifanyika mara kwa mara katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga
mkoani Pwani.
“Mtulia
aliuawa akiwa anaelekea bafuni kuoga. Walimvamia wakampiga risasi na
kupoteza maisha. Hili tukio limetokea kweli ameuawa. Ila marehemu
hakuwa katibu wa chama wa tawi, alikuwa kiongozi miaka ya nyuma sielewi
alistaafu lini,” alisema.
Alibainisha kuwa sababu za mauaji hayo hazijafahamiaka, licha ya wauaji hao kuacha ujumbe wa maandishi.
“Katika ujumbe huo wauaji walidai kuwa marehemu alikuwa mtu wa kudhurumu. Ila hawakusema alidhulumu lini na alimdhulumu nani,” alisema.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa watu waliofanya mauaji hayo, mpaka jana jioni hakuna mtu aliyekamatwa.
“Tunaendelea na msako. Nawataka tu wananchi kuwa watulivu katika kipindi hichi ambacho tunaendelea kuwasaka wauaji,” alisema.
Hivi
karibuni Jeshi la Polisi liliwaua watu wanne wanaosadikiwa kuhusika na
mauaji ya askari polisi wanane na uporaji wa silaha katika eneo la
Mkengeni, Kata ya Mjawa, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani. Tukio hilo
lililotokea takribani wiki mbili zilizopita.
Jeshi
hilo lilieleza chanzo cha mauaji ya askari polisi kujirudia mara kwa
mara katika maeneo hayo ya Mkuranga, Rufiji, Ikwiriri na Kibiti kuwa ni
eneo hilo kuzungukwa na pori.
Akizungumza
kuhusu tukio hilo katika Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam,
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya alisema baada ya
majambazi hao kuwaua askari hao walipora bunduki saba na kutokomea
kusikojulikana.
Alisema
baada ya tukio hilo polisi walifanya operesheni na kufanikiwa kutambua
maficho ya muda ambapo katika majibizano ya risasi walifanikiwa kuwaua
watu hao wanne pamoja na kupata silaha nne mbili zikiwa ni za askari
waliouawa na mbili za majambazi hao.
0 comments:
Chapisha Maoni