Tetemeko
la ardhi lililotokea katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Geita na
Kagera, limesababisha kifo cha askari WP Koplo Joyce Jackson wa Kituo
cha Polisi Misungwi.
Mbali ya kifo hicho, pia limejeruhi watu watatu wakiwamo wanafunzi wa Shule ya Sekondari Igokelo na mahabusu mmoja.
Tetemeko
hilo lililotokea jana saa 6:55 mchana na kudumu kwa muda wa dakika
moja, limesababisha taharuki kubwa katika ofisi za Halmashauri ya
Manispaa ya Ilemela na kwa baadhi ya wananchi wa mikoa ya Mwanza na
Kagera ambao walilazimika kukimbilia ofisi zao kwa hofu ya kuangukiwa na
majengo.
Shuhuda
wa tukio hilo ambaye hakutaka kutaja jina amesema walikuwa
wamepumzika nje ya Kituo cha Polisi Misungwi, baada ya kutokea tetemeko
la ardhi na Koplo Joyce alidondoka chini na kupoteza fahamu.
Alisema walimsaidia kumkimbiza hospitali, lakini wakati wanamfikisha alikuwa tayari amefariki dunia.
“Joyce
alianza kazi jana, baada ya kumaliza likizo ya uzazi. Alijifungua kwa
njia ya upasuaji na ameacha kichanga, alikuwa pia anasumbuliwa na
shinikizo la damu (presha),” alisema shuhuda huyo.
Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, Dk. Marcelina Kiemi,
alithibitisha kupokea mwili wa Koplo Joyce na majeruhi ambao ni
wanafunzi wa Shule ya Sekondari Igokelo na mahabusu mmoja.
“Baada
ya kutokea tetemeko la ardhi, nimepokea mwili wa askari polisi wa kike
Joyce Jackson ambaye alikuwa tayari amefariki dunia,” alisema Kiemi.
Dk.
Kiemi, alisema majeruhi watatu; Anna Habi (18) mwanafunzi wa kidato cha
nne, Mathayo Ndalahwa (15) kidato cha kwanza kutoka Shule ya Sekondari
ya Igokelo na mahabusu Mathias Simoni (22) mkazi wa Kijima, wamelazwa na
wote hali zao zinaendelea vizuri.
Mwalimu
wa Shule ya Sekondari Igokelo, Adela Sakoma, alisema wakati tetemeko
hilo linatokea walikuwa darasani, ndipo wanafunzi walianza kukimbizana
kutoka nje kupitia mlangoni ili kunusuru maisha yao.
Alisema baadhi yao walijeruhiwa na kuwakimbizwa hospitalini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alithibitisha kutokea kifo cha Koplo Joyce.
Alisema kwa muda sasa, Koplo Joyce alikuwa akisumbuliwa na tatizo la presha.
“Huyu
WP Koplo Joyce alikuwa na tatizo la presha, wakati tetemeko linatokea
wakiwa wanatoka nje, alianguka ghafla. Wenzake walimsaidia na kumkimbiza
hospitalini na walipomfikisha tayari alikuwa amepoteza uhai,” alisema Kamanda Msangi.
==>Msikilize Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi akiongea hapo chini
0 comments:
Chapisha Maoni