Wakati
Serikali ikiendelea kujipanga kwa vita dhidi ya dawa za kulevya, Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kutotangaza
majina ya watuhumiwa kabla ya kufanyika uchunguzi na kujiridhisha.
Kauli
hiyo imekuja siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda kulaumiwa na watu tofauti kwa kitendo chake cha kutangaza majina
ya watu aliotaka kufanya nao mahojiano kuhusu matumizi na biashara ya
dawa za kulevya.
Wengi
waliokosoa kitendo hicho, hasa wabunge, walisema kutangaza majina ni
kuharibu uchunguzi na pia kunachafua watu kabla ya kuthibitika kuwa
wanajihusisha na dawa hizo na kwamba chombo pekee kinachoweza kumtia mtu
hatiani ni mahakama.
Watu
walioitwa kituo cha polisi jijini Dar es Salaam, wakiwemo wanasiasa,
wafanyabiashara wakubwa, viongozi wa dini na wasanii walihojiwa na
baadhi kupekuliwa majumbani na ofisini kwao kabla ya kwenda kupimwa.
Baadhi ya watuhumiwa hao ni
kiongozi wa kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima,
mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, mfanyabiashara maarufu nchini,
Yusuf Manji na msanii nyota wa filamu, Wema Sepetu.
Akizindua
Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya uliofanyika ofisi ya
waziri Mkuu jana, Majaliwa alisema wakuu wa mikoa wana nafasi nzuri ya
kushiriki katika vita hiyo kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu.
“Wakuu
wa mikoa mna kazi kubwa katika vita hii. Mkiwa wenyeviti wa kamati za
ulinzi na usalama, mpo kwenye nafasi nzuri ya kuendesha vita hii kwa
mujibu wa sheria, kanuni na taratibu,” alisema Waziri Mkuu mbele ya mawaziri ambao ni wajumbe wa Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya na wakuu wa mikoa.
“Jiepusheni
kuwatangaza watuhumiwa kabla hatujafanya uchunguzi. Itakapotokea
uchunguzi umekamilika na kuwakamata watuhumiwa, msisite kuwatangaza
kwenye vyombo vya habari, msiogope. Serikali inawategemea na itaendelea
kuwaunga mkono,” alisema.
Pamoja
na hayo, Majaliwa alisema Serikali haitawavumilia watendaji wa mamlaka
watakaochukua rushwa kwa lengo la kuwasaidia wahusika wa dawa za
kulevya.
Alisema anafahamu kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni vita kubwa na hilo linatokana na kuhusisha wafanyabiashara wakubwa na watu maarufu.
Alisema anafahamu kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni vita kubwa na hilo linatokana na kuhusisha wafanyabiashara wakubwa na watu maarufu.
“Watendaji
wa mamlaka kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kufahamu kuwa
mmeaminiwa, hivyo muwe waadilifu kwani mmekabidhiwa makubwa yanayohitaji
uangalifu wa hali ya juu,” alisema.
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuendelea kuimarisha mapambano
dhidi ya udhibiti wa dawa hizo nchini na hilo litafanyika bila uonevu
wala upendeleo.
“Dawa
za kulevya ni tatizo kubwa. Tanzania imekuwa ikitumika kama njia ya
kupitishia dawa hizo, hivyo mapambano yanapaswa kufanyika kwa nguvu
kubwa. Sheria ya udhibiti isimamiwe kikamilifu; masharti yote
yaliyotajwa yatekelezwe bila kumuonea mtu,” alisema Majaliwa ambaye kwa nafasi yake anakuwa mwenyekiti wa baraza hilo.
Alisema baraza hilo lina wajibu wa kusimamia utekelezaji wa sera ya udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
Alisema baraza hilo lina wajibu wa kusimamia utekelezaji wa sera ya udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
“Jukumu
hili ni kubwa. Sisi kama wajumbe wa baraza tunatakiwa kulitekeleza kwa
uadilifu na umahiri mkubwa. Sina shaka na wajumbe,” alisema.