Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa zuio la muda kuzuia Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe asikamatwe na
Polisi hadi maombi yake, aliyoyaomba ya kutaka asikamatwe,
yatakaposikilizwa kesho.
Katika
kesi hiyo ya kikatiba namba 1 ya mwaka 2017, Mbowe anapinga mamlaka ya
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalum, Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo (ZCO), Camilius
Wambura, ya kutaka kumkamata hadi maombi hayo yatakaposikilizwa.
Maombi
ya kesi hiyo yataanza kusikilizwa Februari 23, mwaka huu saa 7:30
mchana katika chumba cha wazi cha mahakama ili kuruhusu watu mbalimbali
kusikiliza kesi hiyo.
Jopo
la majaji watatu likiongozwa na Sekieti Kihiyo akisaidiana na Jaji
Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Kaday lilitoa zuio hilo, hata hivyo
walisema Polisi wanaweza kumuita Mbowe kwa mahojiano pindi
watakapomhitaji.
Kesi
hiyo ambayo ilisikilizwa kwa vipindi vitatu kuanzia saa 4 asubuhi hadi
saa 7 mchana, mahakama iliamuru upande wa wadai ambao uliongozwa na
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, kurekebisha maombi yao kwa
kuwa hawakumuingiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) licha ya
kuishitaki serikali.
Hali
hiyo ilitokana na mawakili wa upande wa wadai, Lissu ambaye alipinga
kitendo cha Mwanasheria wa Serikali, Gabriel Malata kuwatetea wadaiwa
hao ambao ni RC, RPC na ZCO katika kesi hiyo kwa kuwa hawajaitaja
serikali.
Akijibu
hoja hiyo, Malata alidai kuwa waliofunguliwa madai hayo sio Makonda,
Sirro wala Wambura, bali ni serikali hivyo ana mamlaka yote ya
kuwawakilisha.
Baada
ya pande zote kuwasilisha hoja zake, mahakama ilimruhusu Malata
kuendelea kusikiliza kesi hiyo ambapo pia iliagiza upande wa wadai
kufanya marekebisho ya maombi hayo na kumuongeza AG kama mdaiwa.
Hata hivyo, Lissu aliomba waruhusiwe kufanya marekebisho hayo kwa kumuongeza AG, ombi ambalo halikuwa na pingamizi.
‘’Tutafanya
marekebisho ya maombi yetu na marekebisho mengine madogo madogo kwa
namna tutakavyoona inafaa siku ya Jumatatu na tutawapa wajibu maombi
Machi 6 mwaka huu na Machi 8 mwaka huu itatajwa kwa ajili ya kusikiliza
maombi hayo,’’ alidai Lissu.
Mbowe
aliwasili mahakamani hapo akiwa na gari lenye usajili namba T 830 aina
ya Land Cruiser, saa chache kabla ya kesi yake kuitwa katika chumba
namba 64 kwa ajili ya kusikilizwa.
Mbowe
ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro, alifika mahakamani hapo
baada ya kutoka Kituo Kikuu cha Polisi saa 7 usiku, alikokuwa anahojiwa
na kupekuliwa kuhusu sakata la dawa za kulevya.
Aidha,
viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiwemo Mbunge wa Kibamba, John
Mnyika, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, Mbunge wa Iringa Mjini,
Mchungaji Peter Msigwa, madiwani na wafuasi wao walijitokeza kwa wingi,
kusikiliza kesi hiyo huku wakifurahia amri ya mahakama ya kuzuia
kutokamatwa kwa mwenyekiti huyo.
Katika
kesi ya msingi, Mbowe anaomba mahakama iwazuie wadaiwa kutekeleza azma
yake ya kumtia mbaroni, pia itoe amri ya kuwazuia kumkamata hadi hapo
kesi hiyo ya kikatiba, itakapomalizika na kwamba polisi wasiendelee na
mchakato wowote dhidi yake hadi hapo kesi hiyo itakapomalizika.
Anadai
kuwa sheria inayompa Mkuu wa Mkoa mamlaka ya kutoa amri ya kumkamata na
kumweka ndani mtu, iko kinyume cha katiba, kwa madai kuwa ilitungwa
katika mazingira ambayo hapakuwa na vituo vya polisi vya kutosha.
Pia anadai kuwa kwa mazingira ya sasa, sheria hiyo imeshapitwa na wakati na anaiomba mahakama itamke kuwa ni kinyume cha katiba.
Mbowe
pia anadai kuwa hata kama Mkuu wa Mkoa alikuwa anatekeleza mamlaka yake
kwa mujibu wa sheria hiyo, basi hakutimiza matakwa ya kisheria, ambayo
ni pamoja na kutoa taarifa kwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya au ya Hakimu
Mkazi.
Vile
vile, anaiomba mahakama kama itaona kuwa Mkuu wa Mkoa alikuwa sawa
kutoa amri hiyo, basi imwamuru afuate matakwa ya kisheria, ikiwa ni
pamoja na kulinda haki za binadamu katika kutekeleza madaraka yake hayo.