Aidha kimeitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti dhidi ya baa la njaa.
Hatua
ya chama hicho inafuatia kile ilichoeleza kutoridhishwa na hatua ya
Serikali katika kuzuia baa la njaa, huku ikikikusanya takwimu ya bei za
vyakula nchini.
Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii wa chama hicho, Janeth Rithe alieleza hayo jana Dar es Salaam.
Alisema
hali ya chakula nchini bado haijatengamaa na kwamba ACT hakiridhishwi
na hatua ambazo Serikali imechukua katika kuzuia tishio hilo la baa la
njaa.
“Tumeshtushwa
na taarifa mpya za Serikali juu ya hali ya chakula nchini, hasa juu ya
uhaba wa vyakula, tishio la baa la njaa na mfumuko mkubwa wa bei za
vyakula, na hali ya ukuaji wa kiuchumi wa wananchi kwa ujumla,”alisema.
Alisema
Sekretarieti ya ACT ilikusanya takwimu kwa wiki mbili kuhusu bei ya
vyakula mbalimbali nchini na kubaini bei ya unga, maharage na vyakula
vingine imepanda kwa takriban Sh1,100 kutoka Sh 900 kwa kilo kwa miezi
mitatu iliyopita hadi Sh 2000 mwezi huu.
Rithe
alisema uamuzi wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi(CCM) kwa kupunguza
bajeti ya ruzuku ya mbolea kutoka Sh. bilioni 78 mwaka 2015/16 hadi Sh.
bilioni 10 mwaka 2016/17 haukuwa sahihi na kwamba sasa inapaswa
kuchochea tija kwenye kilimo.
“Uamuzi
huo umechangia kuwapunguzia wananchi uwezo wa kuzalisha.Takwimu
zinaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotumia mbolea kwa
kiwango kidogo zaidi ulimwenguni.
“Ni
kwa sababu hii takwimu za Serikali zilizotolewa na Waziri wa Fedha
zinaonesha kuwa kwa mwaka 2016 kasi ya ukuaji wa kilimo imeshuka kutoka
asilimia 2.5 hadi 0.6,”alisema.
Alisema
Serikali inapaswa kutenga fedha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili
kupunguza utegemezi wa kilimo cha mvua zisizotabilika.
Kwa mujibu wa ACT, Serikali inatakiwa kujenga maghala ya kutosha pamoja na Bunge kuongeza bajeti ya hifadhi ya Chakula ya Taifa.
Kuhusu
Benki Kuu, ACT ilisema taarifa za benki hiyo kuhusu hali ya uchumi wa
nchi kwa Desemba 2016 zinaonesha kuna mfumuko mkubwa wa bei za vyakula,
hasa chakula kikuu kwa Watanzania.
Alitaja
baadhi ya vyakula kama mahindi, ambapo mfumuko wa bei yake umekua kwa
zaidi ya asilimia 30 na kusababisha kupanda kwa gharama za maisha za
wananchi wote.