Jeshi
la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Patrick Malindisa (29) mkazi wa
Mtaa wa Namanyigu Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kumuua baba yake
mzazi Athanasi Malindisa (70) kwa kumpiga na kitu chenye ncha kali
kichwani na kidevuni na kisha kutaka kuufukia kwenye shimo alilochimba
ndani ya nyumba yao.
Mmoja
wa wanafamilia ambaye ni mdogo wa marehemu Pius Malindisa jana alisema
walipata taarifa ya kifo cha ndugu yao Januari Mosi mwaka huu saa 1:30
jioni kutoka kwa mtoto wa marehemu Patrick Malindisa.
Alisema
marehemu alikuwa akiishi na mtoto wake huyo ambapo baada ya kufanya
mauji hayo alianza kuwaarifu ndugu kuwa amefariki kwa ugonjwa wa tumbo.
Kutokana
na taarifa hizo ndugu walikusanyika nyumbani kwa marehemu ambapo baada
ya kuingia ndani walikuta akiwa amelala ndipo walipowaita viongozi wa
mtaa na baada ya kufunua walibaini marehemu ameuawa kwa kupinga na kitu
chenye ncha kali kichwani na kidevuni.
“Baada
ya kufanyika kwa uchunguzi wa awali tulitoa taarifa polisi ambapo
walifika na kuuchukua mwili kwa uchunguzi zaidi. Na mwili wa marehemu
umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma huku mtoto wake
akishikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.
“Tulipofika
hapa tulikuta shimo limechimbwa ndani ya nyumba na inaelekea
lilimshinda na kuamua kuanza kutoa taarifa kwetu ambapo alidai alikuwa
anaumwa ugonjwa wa tumbo,” alisema Pius
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji amethibitisha kutokea kwa
mauaji hayo ambapo kwa sasa wanamshikilia mtoto wa marehemu, Patrick
Malindisa kwa uchunguzi zaidi.