Jina
la waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa limetajwa na mkaazi mmoja wa
Mbeya mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla kuwa sababu ya deni la
shilingi milioni moja kutokana na mapenzi ya wafuasi wake.
Mkaazi
huyo wa kata ya Ruanda Nzovwe aliyejitambulisha kwa jina la Amos
Mwakyambiki alidai kuwa wafuasi wa Chadema waliharibu paa la nyumba yake
walipopanda kwa lengo la kufuatilia mkutano wa Lowassa wakati wa
uchaguzi mkuu wa mwaka jana, na kwamba chama hicho kilimuahidi kumlipa
fidia ya shilingi milioni moja lakini hadi sasa ahadi hiyo
haijatekelezwa.
Alimueleza
mkuu wa mkoa huo kuwa kutokana na uharibifu huo mkubwa uliofanyika,
wapangaji wake waliamua kuhama nyumba yake hivyo kukosa kipato.
“Naomba
Serikali ya Mkoa inisaidie kuzungumza na meya (wa Chadema) ili niweze
kulipwa stahiki zangu kwani sasa sijui hatma yangu. Kuku niliokuwa nauza
kwa ajili ya kupata nauli kwenda ofisi za jiji wamekwisha,” Mkaazi huyo
anakaririwa.
Kutokana
na madai hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya alimuagiza Mkuu wa Wilaya
kufuatilia suala hilo huku akitahadharisha wananchi kuhusu matumizi ya
nyumba zao wakati wa kampeni.
“Lakini na nyie wananchi msikubali nyumba zenu zibadilishwe kuwa viwanja vya siasa,” alisema Makalla.
Akizungumzia
taarifa hizo, Mkuu wa Idara ya Habari ya Chadema, Tumaini Makele
alisema kuwa chama hicho kitafuatilia kuona ni nani aliyetoa ahadi hiyo
kwa mwananchi huyo na ilikuwa katika mazingira gani ili walifanyie kazi
ipasavyo.