WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Siku ya Maulid
ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambayo kitaifa itaadhimishwa
mkoani Singida.
Katibu
wa Bakwata Mkoa wa Singida, Alhaji Buruhani Mlau alisema sherehe za
Kitaifa za Maulid ya Mtume Mohammad (SAW) kwa mwaka huu zinatarajiwa
kufanyika Mkoani Singida katika Kijiji cha Shelui, wilayani Iramba,
Singida.
Wiki
iliyopita, akitangaza utaratibu wa sherehe hizo, Mufti wa Tanzania,
Sheikh Abubakar Zubeir alisema kwa mwaka huu, Maulid itasomwa usiku wa
Desemba 11 na mapumziko yatakuwa siku inayofuata yaani Desemba 12.
Mufti wa Tanzania aliwataka Waislamu wote nchini waadhimishe Siku ya Maulid kwa kufanya usafi, kupanda miti na kuchangia damu.
“Waislamu
wanatakiwa kutumia siku hiyo kwa kufanya matendo mema na yenye
kumpendeza Mwenyezi Mungu ikiwa ni pamoja na kufanya usafi kwenye mitaa
yao na kuchangia damu ili kusaidia wenye uhitaji huo,” alisema.