MTUHUMIWA
wa uhalifu sugu kutumia silaha za jadi, unyang’anyi na mauaji,
aliyetoroka chini ya ulinzi wa Polisi mwanzoni mwa wiki, Shukuru Jokeri
(25) mkazi wa kata ya Chamwino, Manispaa ya Morogoro, ameuawa na
wananchi baada ya kumkuta akiwa mtaani.
Wananchi walimkuta juzi
Desemba 13 na kisha kumshambuliwa vikali na baadaye kufariki dunia
akipatiwa matibabu hospitalini baada ya polisi kumnasua mikononi mwa
wananchi waliokuwa wakimpiga.
Kamanda wa Polisi wa
mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na
alisema alifariki wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Morogoro.
Alisema mtuhumiwa huyo
alikamatwa na wananchi wa mtaa wa Chamwino, kata ya Chamwino, Manispaa
ya Morogoro, Desemba 13, mwaka huu saa 4 :45 usiku.
Kamanda Matei alisema baada ya kugundua kwamba ndiye aliyetoroka Polisi walimkamata na kumshambulia.
Alisema mtuhumiwa huyo
Desemba 8, mwaka huu, alikamatwa kwa kosa la mauaji na unyang’anyi wa
kutumia silaha aina ya panga na kufikishwa Polisi na alipokuwa
anaendelea kuhojiwa, Desemba 12, mwaka huu alitoroka.
Hata hivyo, alisema
Desemba 13, mwaka huu mtuhumiwa huyo alionekana uraiani ambapo wananchi
walipomwona waliamua kumkamata na kumshambulia.