MWANZA
ni hatari. Ndivyo alivyosema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed
Msangi, baada ya matukio mawili yaliyotokea usiku wa kuamkia jana,
likiwamo la nyumba moja kukutwa silaha za kivita, za jadi na watoto 10
waliokuwa wakifundishwa mafunzo yanayoashiria kuwa ni ya kigaidi.Silaha
zilizokutwa katika nyumba hiyo iliyopo Bugaka, Kata ya Kishili jijini
Mwanza, ni bunduki aina ya AK 47, mabomu ya kurusha kwa mkono, bunduki
aina ya Maker 4, risasi zaidi ya 150, majambia na
visu.Akizungumza na MTANZANIA Jumapili katika mahojiano maalumu, Kamanda
Msangi alisema kuwa aliongoza vijana wake kufika katika nyumba hiyo
baada ya kupata taarifa kutoka kwa baadhi ya watuhumiwa wanaowashikilia
kwa matukio mbalimbali, kwamba wafadhili wao wapo Kishili na Buhongwa.
Msangi
alisema kutokana na taarifa hizo, aliunda vikosi viwili kufanya
operesheni maalumu usiku wa kuamkia jana, kimoja kilikwenda eneo la
msitu wa Deo uliopo Buhongwa na kingine Kishili.
Akizungumzia
kikosi cha Kishili alichokiongoza, alisema walipofika katika nyumba
hiyo waliizingira na watu waliokuwamo ndani wakaanza purukushani za
kutaka kujihami ndipo askari walilazimika kufyatua risasi moja
kuwatuliza.
Kamanda
Msangi alisema wakati wanatafuta namna ya kuingia ndani ya nyumba hiyo
iliyo na uzio, kijana mmoja alifanikiwa kuruka ukuta kwa upande wa nyuma
na kutoroka, lakini wakafanikiwa kuwadhibiti wenzake zaidi ya 15.
“Baada
ya kuwadhibiti na kuingia ndani, tulifanya ukaguzi na kufanikiwa kupata
mabomu ya kurusha kwa mkono yaliyokuwa yameandaliwa kwa matumizi,
bunduki za kivita aina ya AK 47, magazine tano na kila moja ikiwa na
risasi 30, majambia, bunduki ndogo aina ya Maker 4, visu na gari moja
ambayo inawezekana ndiyo wanayotumia kufanya doria zao kabla ya kufanya
matukio.
“Tulipoingia
tumewakuta watoto wadogo 10 waliokuwa wakifundishwa mafunzo maalumu ya
namna ya kutumia silaha walizokuwa nazo na namna ya kujilinda na adui,
pia kulikuwa na wanaume wanne wakubwa na wanawake wawili ambao inaelezwa
ndio watoaji mafunzo kwa watoto hao.
“Katika
mahojiano ya awali, tumeelezwa kwamba watu hao wana vikosi katika mikoa
mbalimbali ya Kanda ya Ziwa, ikiwamo Tabora, Mwanza na Kigoma,”
alisema.
Kamanda
Msangi alisema wakati wanapambana na watuhumiwa hao, wananchi
walijikusanya eneo hilo, wakiwa na nia ya kutaka kuwaua watuhumiwa hao,
lakini askari walisimama imara na kufanikiwa kuondoka nao wakiwa hai.
Alisema
baada ya kuondoka na watuhumiwa hao, baadaye alipata taarifa kwamba
wananchi waliamua kuteketeza nyumba hiyo kwa moto alfajiri ya jana.
WAWILI WAUAWA
Akizungumzia
kikosi cha pili kilichokwenda msitu wa Deo, alisema kiliambatana na
vijana wanne ambao baadhi yao ni waendesha bodaboda, waliokuwa
wakishikiliwa kwa matukio ya hivi karibuni.
Alisema
walipofika katika msitu huo, walionyesha silaha zilipo na katika
ukaguzi walifanikiwa kupata bunduki moja aina ya SMG, magazine mbili
huku moja ikiwa na risasi 15 na nyingine 30, pia walikamata bastola
moja.
“Wakati
askari hao wakifanya upekuzi katika msitu huo, ghafla watuhumiwa hao
walianza purukushani ya kutaka kutoroka, ndipo askari waliwafyatulia
risasi na kuwaua wawili.
“Tunaendelea
kuwahoji watuhumiwa ili kupata mtandao wote, lakini hapa Mwanza ni
hatari, kibaya zaidi vijana hawa wa bodaboda wanajihusisha na vitendo
hivi, tunaomba wananchi kuwa makini na kundi hili,” alisema.