Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa
muda wa miezi Mitatu kwa halmashauri zote nchini kurudisha serikalini
haraka maeneo ya michezo yalivamiwa na watu kwa ajili ya kufanya
shughuli zao binafsi ambapo pia ametoa agizo kuwa kila Jumamosi ya pili
ya mwezi iwe ni siku ya mazoezi kwa watanzania wote ilikujiimalisha afya
zao.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo baada ya kushiriki matembezi na kuzindua wa kampeni ya Kitaifa ya kudhibiti Magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwenye viwanja wa Leaders Club jijini Dar es Salaam.
Makamu
wa Rais ameonya kuwa kama watendaji wa mikoa na halmashauri
watakaoshindwa kurudisha maeneo hayo basi watenge haraka maeneo mengine
kwa ajili ya wananchi kufanya mazoezi kama hatua ya kukabiliana na
magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Katika
kuunga mkono utaratibu wa kufanya mazoezi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi wa mikoa
na wilaya zote kuweka utaratibu wa kufanya mazoezi angalau kwa mwezi
mara Moja.
“Nitamke
kuwa kila Jumamosi ya pili ya mwezi itakuwa siku ya mazoezi kwa afya
kwa sababu mazoezi ni afya na nawaasa wananchi kufanya mazoezi na
kuanzisha na kujiunga na vikundi vya mazoezi na serikali itatimiza
wajibu wake wa kuweka mazingira mazuri ya kufanyia mazoezi kote nchini”
Makamu
wa Rais pia ameagiza watendaji wa Wizara ya elimu, Sayansi na
Teknolojia kurudisha mchakamchaka mashuleni kulingana na maeneo yalivyo.
Amesema mchakamchaka utasaidia kuimarisha afya za wanafunzi na
kukabiliana na magonjwa mbalimbali.
“Natoa
rai utaratibu wa mchakamchaka katika shule zetu urudishwe mara Moja
katika Muda ambao utaonekana ni mwafaka kwa shule husika”.
Katika
hatua nyingine, Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Afya kukamilisha
haraka mchakato wa kuunda kamati ya kushughulikia magonjwa yasiyo ya
kuambukiza itakayojumuisha wadau kutoka wizara mbalimbali nchini.
Amesisitiza kuwa mchakato huo ni lazima ukamilike tarehe 1 machi mwaka 2017.
Kwa
upande wake, Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Ummy Mwalimu amesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza yamekuwa
yanaongezeka sana duniani kote hasa kwenye nchi zilizo chini ya Jangwa
la Sahara ikiwemo Tanzania ambapo magonjwa hayo mpaka sasa yanachangia
asilimia 27 ya vifo Duniani.
Amesema
utafiti uliofanyika mwaka 2012 uliohusisha wilaya 53 hapa nchini
umeonyesha viashiria hatarishi vya magonjwa hayo ambapo asilimia 26 ya
wananchi ni wanene kupita kiasi,asilimia 26 wana lehemu nyingi mwilini
na asilimia 25.9 wanashinikizo kubwa la damu.
Utafiti
huo pia ulionyesha kuwa asilimia 15.9 ya wananchi wanavuta sigara na
asilimia 97.2 ya wananchi wanakula mboga mboga na matunda chini ya mara
tano kwa siku.
Waziri
wa afya Ummy Mwalimu amesema watanzania wanaweza kukabiliana na
magonjwa hayo kwa kufanya mazoezi ya viungo angalau mara tatu kwa wiki
kwa muda wa nusu saa, kuzingatia ulaji wa vyakula unaofaa,kupunguza
matumizi ya pombe kupita kiasi na kujiepusha na matumizi ya tumbaku.
Kwa
upande wake Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi
katika nasaha zake amewahimiza Watanzania kufanya mazoezi kwa ajili ya
kulinda afya zao.
Amesema
kama watanzania watafanya mazoezi wataepukana na magonjwa yasiyo ya
kuambukiza ikiwemo ugonjwa wa moyo,kisukari,uti wa mgongo na mifumo ya
neva na figo.
Kauli mbiu ya uzinduzi wa kampeni ya Kitaifa ya Kudhibiti Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza ni “Afya yako,Mtaji wako”