Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kilimanjaro,
imebaini ufisadi wa zaidi ya Sh bilioni 2.6 katika tuhuma 18
zilizohusisha viongozi waandamizi wa Serikali, vyama vya ushirika,
viongozi wa kisiasa na mawakili.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Alex Kuhanda,
taasisi hiyo ilipokea jumla ya tuhuma 72, ambazo baada ya kuchunguzwa,
41 zilithibitika.
Kuhanda
alisema uchunguzi huo ni kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba mwaka
huu, na kwamba maeneo makubwa yaliyolalamikiwa ni vyama vya ushirika,
Saccos, rushwa na udhalilishaji kwenye mikopo ya kibenki, watumishi hewa
na ufisadi wa fedha za Uchaguzi Mkuu ulifanyika Oktoba mwaka jana.
Kuhanda
alisema tuhuma hizo zilihusisha viongozi 18 waandamizi wa Serikali,
vyama vya ushirika, viongozi wa kisiasa, wafanyabiashara na wafanyakazi
wasio waadilifu katika benki.
Alisema
kuwa katika kipindi hicho, taasisi hiyo imeweza kuokoa zaidi ya Sh
milioni 31 kutokana na malipo ya mishahara hewa pamoja na miamala
mingine.
Kuhanda alisema kwamba muda mwafaka ukifika watuhumiwa watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma zinazowakabili.