Baada
ya Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza kutupilia mbali maombi ya wananchi
wanne wa kutaka itengue ushindi wa Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini Ester
Bulaya (Chadema), walalamikaji hao wamesema watakata rufaa katika
Mahakama ya Rufaa kwa kile walichosema kuwa Mahakama hiyo haikutenda
haki katika kutoa maamuzi hayo.
Novemba
18, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza iliyokuwa inasikiliza kesi
hiyo namba moja ya mwaka huu, katika Mahakama ya Mkoa wa Mara mjini
Musoma, chini ya Jaji Noel Chocha, ilitupilia mbali kesi hiyo na
kumthibitisha Bulaya kuwa ni Mbunge halali wa jimbo hilo.
Wananchi
hao wanne walikuwa wamefungua kesi hiyo wakipinga ushindi wa Bulaya
dhidi ya Stephen Wasira kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.
Baada
ya hukumu hiyo kutolewa waandishi wa habari walimhoji mmoja wa
walalamikaji Janes Ezekiel, ambaye alisema kuwa watakaa na wenzake waone
namna ya kukata rufaa.
Hata
hivyo baadaye mlalamikaji mwingine Ascetic Malagila alimwambia
mwandishi wa habari hii kuwa tayari wamekubaliana na wenzake pamoja na
mwanasheria wao kuwa watakata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kupinga
hukumu hiyo, kwa kile alichoeleza kuwa wameshindwa kwa sababu ya uonevu
na kwamba watatafuta haki yao katika Mahakama ya Rufaa.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, Wasira alidai kuwa tayari walalamikaji hao
pamoja na wakili wao Constantine Mutalemwa, wamekutana na kukubaliana
kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kutafuta haki.
Kabla
ya hukumu hiyo kutolewa Jaji Chocha, alirejea baadhi ya vifungu vya
sheria pamoja na hoja mbalimbali zilizotolewa na waleta maombi
(walalamikaji) na wajibu maombi wa kwanza, wa pili na watatu.
Jaji
Chocha alisema kuwa kutokana na kupitia vifungu vyote vya sheria pamoja
na ushahidi uliotolewa na waleta maombi katika Mahakama hiyo, ni kwamba
ushahidi wao haujajitosheleza katika hatua ya kutengua ubunge wa jimbo
hilo.
Alisema
kuwa iwapo ataamua kufuta matokeo hayo atawasababishia wananchi wa
jimbo hilo ambalo ni miongoni mwa jimbo lenye watu masikini sana kukosa
haki yao.
Alisema
kuwa madhara ya kurudia uchaguzi ni makubwa sana, sanjari na gharama za
uendeshaji wa uchaguzi mpya, ambao utaligharimu taifa na wananchi kwa
ujumla kwa sababu gharama za uchaguzi ni sehemu ya kodi ya kila
mwananchi.
Akirejea
mwenendo mzima wa kesi hiyo tangu ilipofunguliwa katika Mahakama hiyo,
Jaji huyo alikiri kutokea kwa kasoro kadhaa katika kipindi cha uchaguzi
hadi kutangaza matokeo na kusema kuwa ni kawaida ya uchaguzi wowote kuwa
na kasoro ndogondogo na kuongeza kuwa hata nchi zilizoendelea kasoro
huwa hazikosekani.
Alisema
kuwa katika kesi hiyo kasoro nyingi zilizojitokeza zimeonekana mara
baada ya matokeo kutangazwa, lakini katika mchakato mzima wa upigaji
kura hakuna kasoro zilizobainishwa, ambazo zingeweza kuonekana kwenye
fomu yoyote ya malalamiko anayokuwa nayo msimamizi wa uchaguzi, ambazo
zingeonesha kuwa uchaguzi haukuwa wa huru na haki. Alibainisha kuwa si
kila kasoro inayojitokeza kwenye uchaguzi inaweza kuathiri matokeo ya
uchaguzi.
Hata
hivyo alisema kuwa pia msimamizi wa uchaguzi huo Lucy Msoffe alifanya
uzembe mkubwa sana wakati alipofika katika hatua ya kuandika idadi ya
wapiga kura na kwamba alipaswa kuwa makini kwa kutokuandika takwimu
kimakosa.
Akizungumza
nje ya Mahakama hiyo wakili wa mjibu maombi Paul Kipeja, alisema
maamuzi yaliyotolewa na Mahakama hiyo waliyatarajia tangu mwanzo wa kesi
hiyo kwa sababu hakukuwa na hoja zozote za msingi za waleta maombi.
Kuhusu
gharama walizotumia katika kesi hiyo wakili Kipeja alisema kuwa watakaa
pamoja na wakili Tundu Lissu, ili waweze kurudishiwa gharama zao zote
walizotumia kuendeshea kesi hiyo.