BALOZI
wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC), Roeland Van de Geer amesema Tanzania ina haki ya kuamua kutosaini
Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara na Jumuiya ya Ulaya (EPA) hadi
itakapojiridhisha manufaa yake.
Alitoa
kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo
mbalimbali vya habari kuhusu masuala mbalimbali pamoja na kujibu maswali
ya wanahabari hao.
Akizungumzia
suala la Tanzania kutosaini mkataba huo wa EPA, ambao nchi wanachama
waliosaini hufanya biashara bila kutoza kodi, Balozi Van de Geer alisema
ingawa wasiwasi wa Tanzania kuwa mkataba huo utadhoofisha juhudi za
nchi za kufufua viwanda vyake, haoni kama kuna ushindani kwenye hilo.
“Ingawa
sioni ushindani unaohofiwa na Tanzania kwenye soko la EPA, lakini
uamuzi wake wa kutosaini ni haki yao na nisisitize kuwa ni vyema
Tanzania isisaini mkataba wowote ambao wana mashaka nao hadi pale
watakapojiridhisha umuhimu wake,” alisema Balozi Van de Geer.
Aliongeza
ni vyema nchi ikachukua muda kujiridhisha badala ya kukimbilia kusaini,
kwa sababu endapo baadaye wataona mkataba huo hauna manufaa na huku
wameusaini, watasononeka hivyo ni vyema wakaupitia na kuona kama una
maslahi kwao.
Awali,
Septemba mwaka huu, Mwenyekiti wa EAC, Rais John Magufuli alisema
viongozi wote kwa pamoja walikubaliana kupewa muda wa miezi mitatu ili
Sekretarieti ya EAC iangalie na kupitia masharti ya EPA kabla ya kusaini
ili kila mmoja afaidike.
Hata
hivyo, katika jumuiya hiyo ya EAC, nchi ambazo tayari zimesaini mkataba
huo ni Kenya, Rwanda na Uganda na nchi zilizobaki ni Tanzania na
Burundi.
Rais
Magufuli alisema katika kikao hicho, walibaini mambo 10 ambayo
yanapaswa kuangaliwa kabla ya kufikia uamuzi kwa maslahi ya nchi na
wananchi.
Mwenyekiti
alitaja mambo ya kuangaliwa kuwa ni kwa namna gani nchi za EAC
zitafaidika, njia gani itatumika kuzuia bidhaa za kilimo na kulinda
wakulima, usawa, makusanyo yatokanayo na bidhaa zitakazoingizwa, Burundi
itasainije huku ikiwa imewekewa vikwazo na EU, kujitoa kwa Uingereza EU
na athari zake, kukosekana kipengele cha kuruhusu nchi nyingine
kujihusisha na nchi za EAC kibiashara, kukosekana ushuru wa forodha na
kipengele cha nchi kujitoa pale inapoona haijaridhika na mkataba.
Rais Magufuli alisema mkataba huo ukisainiwa kwa wakati huu, nchi wanachama zinaweza kuingia kwenye mtego mbaya.
Akizungumzia
kujiondoa kwa Uingereza kwenye EU, Balozi Van de Geer alisema EU bado
iko imara na umoja huo utaendelea kuwa miongoni mwa mataifa yenye uchumi
imara duniani.
Kuhusu
kiwango cha biashara baina ya Umoja wa Ulaya na Tanzania kwa mwaka,
Balozi Van de Geer alisema hivi sasa mauzo yamefikia dola za Marekani
bilioni mbili kwa mwaka huku akimsifu Rais Magufuli kwa sera yake ya
viwanda na kusema umoja huo unamuunga mkono.
Aidha,
aliisifu Serikali ya Awamu ya Tano kwa kujitahidi kuendesha nchi kwa
kutumia vyanzo vya mapato vya ndani kwa wingi, badala ya bajeti
kutegemea wahisani wa nje.
“Tumeona
juhudi za serikali kwenye suala la bajeti ya sasa utegemezi wa wahisani
kutoka nje ni chini ya asilimia 15 ya bajeti, ukilinganisha na awali
ambapo bajeti kwa asilimia 40 ilikuwa tegemezi kwa wahisani, tunaona
mabadiliko, na hii inaifanya Tanzania kuondoka kwenye nchi za kundi
masikini zaidi duniani,” alieleza.