Mtu
mmoja anayehusishwa na vitendo vya ugaidi, Azan Abubakary amefikishwa
katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini na kusomewa mashtaka yake.
Akiwa
amevalia fulana ya rangi ya bluu na kijani na suruali nyeusi na viatu
vya matairi (maarufu kama katambuga), alisomewa shtaka lake mbele ya
Hakimu Mwajuma Lukindo.
Mshtakiwa
huyo anashtakiwa kwa makosa ya kufadhili ugaidi chini ya kifungu cha 13
cha sheria ya makosa ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002.
Ilidaiwa
kuwa Mei 15, 2016 alimtumia fedha Mohamed Ibrahim kwa njia ya M-Pesa
kiasi cha Sh 265,000 katika namba +254 708104109 kwa ajili ya kufanyia
ugaidi nchini.
Aidha
Julai 22, 2016 Abubakary alionekana eneo la Dodoma akituma fedha kwa
njia ya M-Pesa kwa Mohamed Ibrahim Sh 148,000 kwa ajili ya kufanya
vitendo vya ugaidi.
Hakimu Lukindo alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Jeshi
la Polisi Mkoa wa Dodoma katika taarifa yake kwa vyombo vya habari
imesema kwamba mtuhumiwa huyo aliyefikishwa mahakamani ni mwanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Kitivo cha Afya na yupo mwaka wa pili.
Taarifa
hiyo iliyosainiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro
Mambosasa, mtuhumiwa alikamatwa Nzega mkoa wa Tabora baada ya
kugundulika kuwa anajihusisha na mtandao wa ugaidi wa kundi la ‘Al
Shabaab’ kutoka Somalia.
Kamanda alisema mtuhumiwa alikamatwa kutokana na taarifa za Intelijensia ya Polisi katika masuala ya ugaidi.