Rais wa Zambia, Edgar Lungu amewataka watendaji wa nchi yake na Tanzania, kuweka siasa pembeni na kujikita kwenye biashara zitakazoinua uchumi wa nchi hizo mbili.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa kuhitimisha ziara yake ya siku tatu, Rais Lungu aliyetembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Kusafirisha na Kupokea Mizigo la Zambia (Zamcargo), alisema licha ya kuenzi mchango wa waasisi wa mataifa hayo, Mwalimu Julius Nyerere na Kenneth Kaunda, watajikita zaidi kwenye biashara.
“Changamoto mliyonayo ni kwenu uongozi na Bodi ya TPA kwa watu wa Kusini au Mashariki au hata nje ya Afrika. Watu wa Zambia wanasema muda wa siasa umekwisha, sasa ni muda wa maendeleo. Hatutawaunga mkono kwa sababu niko karibu sana na Rais (John) Magufuli. Ni kweli niko karibu na Rais Magufuli kama mlikuwa hamjui, lakini hatuwaungi mkono kwa sababu hiyo, bali kwa ufanisi wenu,” alisema Rais Lungu.
Akizungumzia miradi ya reli ya Tazara na bomba la mafuta la Tazama, Rais Lungu alisema nayo inapaswa kufanya kazi kwa ufanisi.
“Ni kweli sisi ni ndugu lakini hatuangalii hilo. Wazambia wanataka mbolea ifike haraka, shaba isafirishwe haraka kwenda sokoni,” alisema.
Akiwa katika ofisi za Zamcargo, Rais Lungu alirudia wito wake wa ufanisi wa biashara akisema hatasita kuwawajibisha watendaji wa taasisi hiyo.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alisema Zambia imekuwa mteja namba moja katika usafirishaji wa mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Kakoko alisema mwaka 2014, Zambia ilichangia asilimia 36 ya mizigo ambayo ni sawa na tani milioni 5.2 ikiwa ni mbali ya nchi nane zinazotumia bandari hiyo.
“Takwimu za TPA zinaonyesha kuwa mizigo ya Zambia inayopitia hapa imekuwa ikiendelea kila mwaka. Mwaka 2011, bandari ilipokea tani milioni 1.6 za mizigo inayotoka na kuingia. Lakini mwaka 2014 Zambia ilipokea tani milioni 1.9 za mizigo ya Zambia,” alisema Kakoko.
Alisema kutokana na umuhimu huo, uongozi wa TPA umekuwa ukiboresha huduma ili kufanya kazi kwa ufanisi.
“Kwa mfano, muda wa kutoa mizigo bandarini umepunguzwa hadi siku kumi na moja mwisho wa Oktoba kulinganisha na siku 32 zilizokuwa mwaka 2008. Bandari pia imeboresha mfumo wa malipo ya mizigo kwa wateja wake kwa kutumia mfumo wa kielektroniki,” alisema Kakoko.
Katika ziara hiyo ya bandarini, Lungu aliambatana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa na Kikanda, Balozi, Augustine Mahiga, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani na katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Leonard Chamuriho.
Mara baada ya ziara hiyo Rais Magufuli aliwaongoza viongozi wengine wa Serikali kumsindikiza mgeni wake huyo uwanja wa ndege na kurejea Zambia.
Viongozi wengine waliofika uwanjani hapo ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine. Rais Lungu aliondoka uwanjani hapo saa 7: 40 mchana.