Mwanaume
mkazi wa Ilala, Siwema Seif (40) amehukumiwa na Mahakama ya Mwanzo ya
Ilala kwenda jela mwaka mmoja kwa kumtolea lugha ya matusi na
kumdhalilisha kimwili, Zainab Ramadhan ambaye ni mama yake mzazi.
Akisoma
hukumu mahakamani hapo jana, Hakimu wa Mahakama hiyo, Matrona Luanda
alisema ushahidi uliotolewa na shahidi namba moja ambaye ni mlalamikaji,
ulionesha kukosa shaka na kumtia hatiani mshitakiwa.
Shahidi
huyo alisema siku ya tukio mshitakiwa alifika nyumbani kwao akaomba
chakula akajibiwa kuwa kuna wali na mshitakiwa akasema hataki wali bali
anataka ugali na mama akamjibu asingeweza kupika ugali na kumsisitiza
Siwema ale wali.
Zainab
alisema baada ya majibizano hayo, mshitakiwa alimtukana matusi ya
nguoni mama yake, huku akisema hawezi kumzaa na kumkashifu, kwamba hana
sehemu ya kumzalia huku akitishia kumwua akiahidi kumtoa roho ndipo
amjue yeye ni nani.
Kwa
mujibu wa Zainab, alipoona ugomvi na matusi umezidi aliingia chumbani
mwake, na ndipo mlalamikaji akamfuata na kumtukana huku akitishia
kumwingilia kinyume cha maumbile.
“Baada ya hapo mshitakiwa alinivamia na kunidhalilisha kimaumbile kwa mikono yake,” alisema.
Baada ya ushahidi wa mama huyo dhidi ya Siwema, Mahakama ilitoa nafasi kwa kijana huyo kujitetea na Mahakama ikamtia hatiani.
Karani
wa mahakama hiyo, Blanka Shao alisema kwa kuwa mshitakiwa alikuwa
mkosaji wa mara ya kwanza na kitendo alichokifanya ni cha kifedhuli tena
haonyeshi kujutia, alishauri apewe adhabu kali ili iwe fundisho kwake.
Hakimu Luanda alimhukumu kwenda jela mwaka mmoja kwa kitendo alichomfanya mama yake mzazi.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo, kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 9 Ilala, mtaa wa Sophia Kawawa, nyumba namba 10.