Licha
ya Mkutano wa Tano wa Bunge uliomalizika juzi kuwa mahsusi kwa ajili ya
kamati za kudumu kuwasilisha taarifa za hesabu ambazo aghalabu
hufuatiwa na mijadala mizito hasa ya ufisadi, safari hii haikuwa hivyo,
badala yake hoja sita tofauti na hizo ndizo zilizotikisa vikao vyake.
Mkutano
huo uliofanyika kwa siku 10 na kumalizika juzi, pamoja na mambo mengine
ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kamati hizo kuwasilisha taarifa zao kuhusu
hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) kwa mwaka wa fedha wa 2013/14 na 2014/15 ambazo safari hii
zilipewa umuhimu mdogo ikilinganishwa na mikutano iliyopita.
Kamati
zilizowasilisha taarifa zao ni ya Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za
Serikali za Mitaa (Laac) ambazo licha ya kuibua kashfa kama ya Mfuko wa
Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika Mradi wa Kigamboni na
ukopeshaji wa vikundi vya kuweka na kukopa (Saccos), mradi wa vifaa vya
utambuzi wa vidole uliokuwa ukifanywa na Kampuni ya Lugumi kwa Jeshi la
Polisi na utata wa mizigo kwenye Mamlaka la Bandari Tanzania (TPA),
hayakuonekana kupewa umuhimu mkubwa katika mijadala bungeni.
Mambo
mengine ambayo hayakupewa umuhimu katika mkutano huo wakati wa
majadiliano ni kashfa ya mradi wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda)
na mradi wa machinjio wa jiji la Dar es Salaam. Lakini kuna mambo
ambayo yalipewa kipaumbele.
Ukata bungeni
Wabunge
wengi wakiwamo wa CCM na wale wa upinzani katika michango yao
walijikita zaidi katika hali ya uchumi inayowakabili wananchi pamoja na
Bunge lenyewe wakisema hali hiyo imewafanya washindwe kufanya shughuli
za ukaguzi wa miradi na taasisi za umma.
Mbunge
wa Mpwapwa (CCM), George Lubeleje alisema ni aibu kwa wabunge kukaa
kwenye kamati na kusubiri kuletewa taarifa za miradi na maofisa wa
Serikali badala ya wao kwenda kuikagua ili kujiridhisha na kile
walichoambiwa “Hivi ni nani aliyeua mfuko wa Bunge? Hiki tunachokifanya
hapa ni kuisimamia Serikali au kupitisha tulicholetewa na maofisa wa
Serikali? Hii si sawa hata kidogo ni lazima tuikatae hali hii,” alisema.
Hoja
hiyo, iliungwa mkono na Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche
akisema hata kamati zinazokaa hadi usiku zimekuwa zikikosa huduma ya
maji ya kunywa.
Mikopo
Wabunge
pia walivutana na Serikali kuhusu muda wa urejeshwaji wa mikopo ya
elimu ya juu kwa wanafunzi walionufaika katika Muswada wa Marekebisho ya
Sheria mbalimbali Namba 3 wa mwaka 2016. Katika muswada huo, Serikali
iliwataka wanafunzi hao kuanza kulipa, mwaka mmoja baada ya kumaliza au
kukatika masomo yao.
Katika
mvutano huo ambao wabunge wa pande zote mbili yaani wa CCM na wa
upinzani walizungumza lugha moja na Serikali ililazimika kuongeza hadi
miaka miwili kwa mnufaikaji wa mikopo hiyo kuanza kufanya marejesho.
Mbunge
wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara ndiye aliyepeleka mapendekezo
akitaka Serikali kuongeza muda wa wanufaika hao kuanza kulipa mkopo.
Alisema kinyume chake, wanufaika kutoka familia maskini watashindwa kulipa mikopo hiyo kwa muda huo uliowekwa.
Hoja
ya Waitara iliungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT - Wazalendo),
Kabwe Zitto, Ridhiwani Kikwete (Chalinze - CCM), Ester Matiko (Tarime
Mjini - Chadema), Elibariki Kingu (Manyoni Magharibi - CCM) na Fratei
Massay (Mbulu Vijijini - CCM).
Uzoefu wa ma-DED
Wabunge
pia waliibua mjadala wa uteuzi wa wakurugenzi watendaji wa halmashauri
(DED) na watumishi wengine katika Awamu ya Tano wasiokuwa na uwezo wa
kuongoza maeneo waliyochaguliwa.
Baadhi
ya wabunge walisema wakurugenzi hao walichaguliwa kutoka maeneo tofauti
bila kuzingatia Sheria ya Utumishi wa Umma na uzoefu walionao katika
utumishi huo hivyo kushindwa kuelewa majukumu yao na kujikuta wakivuka
mipaka yao ya kazi na wakati mwingine kutokuwa na ushirikiano na
watumishi.
Mbunge
wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alisema wengi wao hawana uwezo wala
uelewa wa shughuli za Serikali kwa kuwa hawakuwahi kufanya kazi huko na
walipochaguliwa hawakupewa semina yoyote.
Hoja
yake iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Laac, Vedasto Ngombale aliyesema
kamati yake imebaini maofisa wa idara na vitengo kwa baadhi ya
halmashauri kutokuwa na uwezo wa kutosha kutekeleza majukumu yao.
“Kamati
imeshuhudia wakuu wengi wa idara na vitengo wakishindwa kutoa majibu
sahihi na kamilifu mbele ya kamati na kushindwa kuelewa shughuli
zinazofanyika ndani ya idara zao,” alisema.
Tuhuma ya Sh10 milioni
Madai
ya wabunge wa CCM kupewa Sh10 milioni kila mmoja ili wapitishe Muswada
wa Huduma za Habari wa mwaka 2016 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo
kwa mwaka wa Fedha 2017/18, ni moja ya mambo yaliyotikisa Bunge.
Tuhuma hizo ziliibuliwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe wakati akimuuliza swali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Madai
hayo yalisababisha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa Mwaka 2016,
tofauti na miswada mingine ya sheria inayokuja bungeni kutawaliwa na
vijembe baina ya wabunge wa upinzani na chama tawala.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Huduma ya Jamii, Peter Serukamba alisema hakuna mbunge
aliyechangia vifungu vya muswada huo ambaye alilenga katika kupinga
vifungu vya muswada huo na badala yake walijikita katika vijembe tu.
“Mkitaka
kujua muswada huu ni mzuri sikilizeni, hakuna mtu alipinga vifungu kama
yupo mtu asimame wote mliamua kucheza katika siasa tu. Lakini kwa maana
ya sheria yenyewe hakuna mtu aliyeweka neno kwa sababu kila kitu
kimefanywa,” alisema Serukamba.
Mbunge
wa Viti Maalumu (CCM), Juliana Shonza alirushiana maneno na Halima Mdee
(Kawe – Chadema) aliyemtamkia maneno ‘milioni 10 hizo’ baada ya
kuelezea kukerwa kwake na watu wanaoingilia utendaji wa vyombo vya
habari.
Kauli moja ya Epa
Kuhusu
Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Jumuiya ya Ulaya na Afrika
Mashariki (Epa), wabunge wote waliungana kuipinga Serikali wakisema
hauna na masilahi kwa Taifa.
Mbunge
wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda alisema mkataba huo una kila dalili ya
kuirudisha nchi katika ukoloni kwa sababu vifungu vyake kwa zaidi ya
asilimia 80 ni vya ukandamizaji.
Spika, Job Ndugai alipigilia msumari wa mwisho aliposema kwamba haufai.
CAG
Pia,
wabunge wengi walizungumzia suala la CAG kutengewa kiasi kidogo cha
fedha katika mwaka wa bajeti wa 2016/17 jambo ambalo litamfanya akague
taasisi chache na hivyo kuwapa ugumu wabunge kuisimamia Serikali.