Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) imetoa notisi ya siku thelathini kwa wanufaika wa mikopo kulipa madeni yao na kwamba wasipotekeleza hilo watachukuliwa hatua za kisheria.
Mkurugenzi Mtendaji wa HELSB, Abdul-Razak Badru wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, amesema HELSB inadai wanafunzi 142,470 mikopo yenye thamani zaidi ya trilioni 23 na kwamba kati yao kuna waliokopa miaka ya 1993 kabla ya bodi hiyo kuanzishwa ambapo walikopeshwa na Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia .
Miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa kwa wadaiwa hao ni pamoja na majina yao kutangazwa hadharani ili wadhamini, waajiri na wadau wengine wenye taarifa zao waziwasilishe katika bodi. Pia itawasiliana na wadhamini wa wadaiwa ili waziwasilishe taarifa zao na au kuwalipia madeni yao.
Hatua nyingine itakayochukuliwa ni kuwasilisha majina ya wadaiwa sugu kwenye taasisi zinazotunza taarifa za ukopaji ili majina yao yawasilishwe katika taasisi za fedha zote kwa ajili ya kutathmini tabia zao kabla ya kuwakopesha au kuwadhamini.
Aidha,Badru amesema kuwa bodi hiyo iko katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani wadaiwa sugu ili walipe madeni yao na gharama za kuwatafuta pamoja na kuendesha kesi