Baada
ya uamuzi wa kuwafukuza vyuo walimu wanne waliokuwa kwenye mafunzo ya
vitendo katika Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mbeya (Mbeya Day),
serikali imesema vyuo husika vinaweza kushauri adhabu mbadala iwapo
vitajiridhisha kuwepo kwa mazingira tofauti na yaliyozingatiwa kwenye
uamuzi wa kuwafukuza vyuo.
Waziri
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako alisema hayo juzi alipozungumza na waandishi wa habari mkoani
Mbeya alikokuwa katika ziara kwenye shule mbalimbali mkoani humo.
Profesa
Ndalichako alisema uamuzi uliochukuliwa na ofisi yake ulizingatia
sheria ndogo zilizotungwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm)
zinazoainisha makosa yanayoweza kumfukuzisha chuo mwanafunzi.
Hata
hivyo, alisema uamuzi uliochukuliwa unaweza kutazamwa upya na vyuo
husika iwapo uzito uliochukuliwa na wizara utaonekana kuwa katika
mazingira na uhalisia wa tukio husika.
Walimu
wanne waliokuwa kwa vitendo katika shule ya Mbeya Day walifukuzwa vyuo
baada ya uamuzi wa serikali kutokana na kuhusika kumpiga mwanafunzi
Sebastain Chinguku vibao, mateke na fimbo kwa ukatili Septemba 28 mwaka
huu shuleni humo.
Walimu hao walibainika baada ya kipande cha video kusambazwa katika mitandao ya kijamii hivi karibuni.
Waliohusika
na vyuo walivyokuwa wakisoma ni Frank Msigwa (anayedaiwa kumpiga zaidi
mwanafunzi makofi kichwani), John Deo na Sante Gwamaka wote wa
DUCE-UDSM, na Evans Sanga wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere.
Akijibu
swali la idadi ipi ya viboko inastahili kutolewa kama adhabu kwa
mwanafunzi anayekwenda kinyume na maelekezo ya shule yake, Profesa
Ndalichako alisema binafsi asingependa mwanafunzi achapwe hata kiboko
kimoja lakini hilo linawezekana pale wanafunzi watakapozingatia maadili.
“Adhabu
yoyote kwa mwanafunzi inatolewa pale anapokuwa amekwenda kinyume na
maadili ya shule yake. Kama wanafunzi wote watazingatia maadili sidhani
kama kuna mwalimu atakayempiga mwanafunzi hata kiboko kimoja. Haya yote
yanatokea kutokana na wanafunzi kukosa nidhamu,” alisisitiza Ndalichako.
Aliwasihi
wanafunzi kuzingatia maadili ya shule yao, akisema ndiyo njia pekee ya
kuwawezesha kuishi vyema na walimu wao na pia kufanya vyema kitaaluma na
kuwasihi wazazi kuwafundisha watoto wao nidhamu ya kuwaheshimu watu
wote, akisema malezi hayo yatawapunguzia walimu adha ya kuishi na
wanafunzi watukutu ambao kimsingi wanazorotesha utendaji kazi wao.