Aliyekuwa
Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye amesema kuwa
baada ya kutangazwa mchakato wa kunyang’anywa shamba lake la
Mwabwepande, amepata taarifa ya kutaka kuondolewa anapoishi pia.
Sumaye
ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache baada ya Waziri Wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kueleza kuhusu kuanza rasmi kwa
mchakato wa kumnyang’anya mwanasiasa huyo shamba la Mwabwepande kwa
madai ya kutoliendeleza kwa muda mrefu.
“Hapa ninapoishi naambiwa kuna maelekezo yametoka juu kuwa sijapaendeleza. Sasa kama sijapaendeleza mbona ninaishi hapahapa,” Sumaye amekaririwa na gazeti la Nipashe.
Aidha
Sumaye amesema kuwa ingawa alimsikia Waziri Lukuvi akieleza kuwa tayari
wameshampa notisi ya siku 90 kuhusu kunyang’anywa shamba lake la
Mwambwepande, hadi jana hajaipata notisi hiyo licha ya kufanya jitihada
za kuifuatilia.
Alisema
kuwa anashangazwa na uamuzi huo wa Waziri kwani kesi inayolihusu shamba
hilo bado inaendelea mahakamani kutokana na uvamizi wa wananchi na
kwamba Mahakama imezitaka pande zote mbili kutofanya chochote kwenye
ardhi hiyo.
Mwanasiasa
huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema alisema kuwa
anachokifahamu ni kwamba alipokea notisi ya kuondolewa katika shamba
lake la Mvomelo kwa madai ya kushindwa kuliendeleza kwa muda mrefu.
“Ninachokijua
ninaandamwa kisiasa. Shamba langu la Mvumelo naambiwa sijaliendeleza.
Kwenye hilo shamba nimejenga nyumba ya kuishi, ghala, kuna trekta na
vifaa vingine. Ninalima mazao na nimefuga zaidi ya ng’ombe 200, nina
kondoo 300 na nimechimba visima viwili vya maji halafu serikali inasema
sijaliendeleza,” alisema Sumaye.
Alisisitiza
kuwa ingawa anaamini anaandamwa kisiasa kwa kunyang’anywa mashamba
yake, hatarejea CCM hata akinyang’anywa mashamba yote aliyoanayo.
Sumaye
alihama CCM mwaka jana, miezi michache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi
Mkuu na kujiunga na harakati za kumpigia kampeni mgombea urais kwa
tiketi ya Chadema, Edward Lowassa. Baada ya uchaguzi huo alitangaza
kujiunga rasmi na Chadema.