Wakati
polisi ikizuia mkutano mkuu maalumu wa CUF uliopangwa kuhudhuriwa na
Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad mjini Tanga jana,
mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim
Lipumba alifanya usafi soko la Buguruni, huku akilindwa na jeshi hilo.
Lipumba
alifanya kazi hiyo akitekeleza agizo la Rais John Magufuli la kufanya
usafi Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi. Msemaji wa CUF, Abdul Kambaya
alisema haoni kama ni jambo la ajabu kwa Lipumba kufanya usafi wakati
akilindwa.
“Sioni mantiki ya swali hilo, suala la kulindwa Lipumba siyo wa kwanza,” alisema
Mapema
jana, polisi mjini Tanga ilizuia mkutano uliopangwa kuhudhuriwa na
Maalim Seif ambao ulipaswa kuwajadili madiwani 12 waliopigana wiki
iliyopita katika ofisi za chama hicho wilayani humo, baada ya
kugawanyika kuhusu uamuzi wa wenzao waliohudhuria baraza la madiwani wa
jiji hilo Oktoba 12.
Taarifa
ya jeshi hilo ilidai kuzuiwa kwa mkutano huo ni kutokana na tisho la
uvunjifu wa amani na kuwapo kwa makundi mawili yanayozozana. Mkutano huo
ulipangwa kufanyika katika Hoteli ya Mkonge mjini hapa.
Pia,
taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Tanga, Idd Abdallah
ilisema ukumbi ambao mkutano huo ungefanyika ni mdogo kutokana na wingi
wa wanachama.
“Ukumbi
uliopangwa kufanyika kwa mkutano huo ni mdogo na ikumbukwe kuwa wiki
iliyopita mkutano wa chama hicho ngazi ya wilaya ulivunjika kutokana na
vurugu,” alisema
Akizungumzia
sakata hilo, Mwenyekiti wa CUF wa wilaya hiyo, Rashid Jumbe alisema
hata kama jeshi hilo limezuia mkutano huo, lengo la chama kuwajadili
madiwani hao liko palepale.
Alisema
kamati ya utendaji imependekeza madiwani saba kati ya 12 wafukuzwe
uanachama kutokana na kukiuka msimamo wa chama na watano watabaki chini
ya uchunguzi.
“Katika
fagio hili mbunge (Mussa Mbaruku) pia yumo kwani naye alishiriki
kikamilifu pamoja na naibu meya (Mohamed Aniu), kwa sasa tunafanya
utaratibu na jeshi la polisi kutekeleza masharti na vigezo wanavyotaka
ili kuufanya mkutano huo tena,” alisema.