Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutafuta fedha za mafunzo kwa ajili ya wahadhiri wa vyuo vikuu nchini ili kuziba pengo la wahadhiri waandamizi lililopo hivi sasa
Waziri Mkuu pia amevitaka vyuo hivyo viweke utaratibu wa kuachiana nafasi ama kurithishana kazi (succession plan).
Amesema yeye binafsi anatambua upungufu uliopo umesababishwa na masharti ya ajira za mkataba kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Oktoba 25, 2016) wakati akifunga kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyoanza jana kwenye ukumbi wa Nkrumah. Kampasi ya Mwalimu J. K. Nyerere, jijini Dar es Salaam.
“Ninatambua kuwa katika vyuo vya umma kuna upungufu mkubwa wa wahadhiri waandamizi na maprofesa na hivyo kuathiri hali ya utoaji wa taaluma kwa fani za ‘Post-Graduates’. Ninajua kuwa pamoja na sababu nyingine, hali hii inachangiwa pia na masharti ya ajira za mikataba kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70.,” amesema.
Akizungumzia kuhusu maslahi ya watumishi wa vyuo hivyo, kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha inaondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi wote wa umma na hivi sasa inakamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi kwa watumishi wa umma ili kubaini watumishi hewa.
“Hadi kufikia tarehe 20 Oktoba, 2016 zoezi linaloendelea hivi sasa, limesaidia kuwabaini watumishi wa umma hewa wapatao 16,500. Baada ya zoezi hilo, tutarudia uhakiki wa madeni yote yaliyowasilishwa Serikalini na kisha tutalipa madeni ya watumishi wote,” amesema.
Akifafanua kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa taarifa za waombaji wa mikopo. Ametoa wito kwa wanufaika na waombaji wote wa mikopo wahakikishe kuwa wanatoa taarifa zilizo sahihi na za uhakika.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali ilikwishaongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka sh. bilioni 340 mwaka 2015/2016 hadi sh. bilioni 483 kwa mwaka 2016/2017.
Mapema, akielezea utendaji kazi wa chuo hicho katika miaka yote 55, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Rwekaza Mukandala amesema chuo hicho kinakabliwa na changamoto ya uhaba wa wanataaluma waandamizi wa fani mbalimbali.
“Chimbuko la changamoto hii ni kusitishwa kwa ajira katika taasisi za umma kwenye miaka ya 1990. Kutoajiriwa kwa wanataaluma chipukizi kwa miaka mingi, kulivuruga utaratibu wa miaka mingi wa kurithishana uzoefu baina ya wanataaluma wanaostaafu na wale ambao wangelichukua nafasi zao,” amesema.
“Hali hii iko kwenye vyuo vikongwe ambako mamia ya wanataaluma wazoefu wanastaafu kwa wakati mmoja na wengi wa wanataaluma walioajiriwa hivi karibuni bado wako masomoni au wangali chipukizi katika taaluma zao na hivyo hawana uwezo wa kutosha kubeba majukumu ya kufundisha katika ngazi za digrii za umahiri na uzamivu,” amesema.
Wakati huohuo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo alisema wizara hiyo imetenga kiasi cha sh. bilioni 9 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu kwenye chuo hicho zikiwemo maabara.