Hayo yamesemwa
jana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari baada ya taarifa kuhusu Rais kutengua uteuzi wake
kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Mkuu wa mkoa alisema
kuwa alipigiwa simu nyingi na watu wengi lakini kabla hajawajibu Rais
Magufuli akampigia simu na kumueleza kuwa ana imani naye na kuwa
ahakikishe anawatumikia wananchi wa Arusha kwani yeye sio bosi wao bali
ni mtumishi wao.
Pia mkuu wa mkoa alieleza
kuwa Rais amempa maagizo ya kuhakikisha anasimamia wananchi wa mkoa wa
Arusha walipe kodi kwa ajili ya maendeleo ya mkoa huo na nchi kwa
ujumla.
Aidha,
ili kuthibitisha kuwa ni Rais Magufuli ndiye aliyempigia simu, Rais
aliomba kuongea na yeyote aliyekuwa karibu ndipo mkuu wa mkoa akampa
mmoja wa waliokuwa katika mkutano huo kuthibitisha kuwa ni Rais
Magufuli.
Habari ya kutenguliwa kwa mkuu wa mkoa wa Arusha imekuja ikiwa
ni siku moja baada ya kuibuka mvutano mkali kati ya mkuu huyo wa mkoa
na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema kuhusu mradi wa ujenzi wa
hospitali itakayotoa huduma kwa mama na mtoto mkoani humo.