Mrithi
wa Mfalme wa Abu Dhabi na Kaimu Rais, Mtukufu Sheikh Mohamed bin Zayed
Al Nahyan amemuahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe
Magufuli kuwa nchi hiyo imedhamiria kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano
wake na Tanzania hususani katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mtukufu
Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan ametoa ahadi hiyo kupitia kwa
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi Bw. Mohamed Al
Suwaidi aliyekutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli jana tarehe
27 Oktoba 2016.
Mfuko
wa maendeleo wa Abu Dhabi unashirikiana na Tanzania katika utekelezaji
wa miradi mbalimbali na katika mazungumzo ya leo Mkurugenzi Mkuu wa
mfuko huo ameonesha nia ya kushirikiana zaidi na Tanzania katika maeneo
ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo reli na barabara, usafiri wa anga na
madini.
Pamoja
kumshukuru Mrithi wa Mfalme wa Abu Dhabi na Kaimu Rais Mtukufu Sheikh
Mohamed bin Zayed Al Nahyan, Rais Magufuli ameialika nchi hiyo kupitia
mfuko wake wa Maendeleo na wadau wengine wa maendeleo kuja kuwekeza hapa
nchini katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa bandari, ujenzi wa
viwanda, kilimo, uvuvi, gesi na kushirikiana katika ujenzi wa reli ya
kati ambayo itazinufaisha nchi nyingine saba za Afrika Mashariki na kati
ambazo hazina bandari.
“Tanzania
imeamua kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na
tayari katika bajeti yetu tumetenga Shilingi Trilioni 1 kwa ajili ya
kuanza ujenzi, hivyo tunawakaribisha Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi
kushirikiana nasi, wapo wengi ambao wamejitokeza kushirikiana nasi
lakini na nyie pia tunawakaribisha, mnaweza kuchukua sehemu ya reli na
mkaijenga” alisema Rais Magufuli.
Aidha,
Dkt. Magufuli aliutaka mfuko huo kufupisha muda unaotumika katika
mchakato wa kuanza utekelezaji wa miradi ili kuharakisha matokeo yake na
manufaa kwa wananchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU