Rais John Magufuli, amemteua Jenerali Mstaafu George Waitara kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (TANAPA).
Taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi huo umeanza jana.
Jenerali George Marwa Waitara alizaliwa Septemba 15 mwaka 1950 katika Kijiji cha Itirya, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara. Alimaliza masomo yake ya Sekondari katika Shule ya Sekondari Minaki, Dar es salaam mwaka 1969.
Mafunzo ya Jeshi:
Alijiunga rasmi na jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania mwaka 1970 akiwa ofisa mwanafunzi, na alipata kamisheni mwaka 1971, na kuhudhuria mafunzo mbalimbali ya kijeshi.
Uzoefu Jeshini:
Mwaka 1978, katika vita ya Tanzania na Uganda, Waitara alikuwa miongoni mwa makamanda walioongoza vikosi katika vita hiyo.
Waitara alikuwa Mkuu wa Majeshi kuanzia 2001 hadi 2007 kabla ya kupokelewa na Gen. Mwamunyange.
Wakuu wa majeshi wengine waliomtangulia Waitara ni Sam Hagai, Mrisho Sarakikya, marehemu Abdallah Twalipo, David Musuguri, Ernest Mwita Kiaro na Robert Mboma.
Pia, Rais Magufuli amemteua Dkt. Eligy Shirima kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI)
Uteuzi wa Dk Shirima nao umeanza jana.
Kabla ya uteuzi huu Dkt. Shirima alikuwa Mtafiti Mkuu na Msimamizi wa Utafiti wa Nyama ya Ng'ombe Makao Makuu ya Taliri.