test

Jumapili, 23 Oktoba 2016

Magufuli afichua madudu 5 mikopo elimu ya juu



RAIS Dk. John Magufuli ameibua madudu matano yaliyosababisha  kujitokeza kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali nchini kuhusiana na mikopo ya elimu ya juu.
Madudu hayo ni pamoja na utaratibu mbovu serikalini, kutokuwapo kwa uratibu wa kufungua vyuo, mawasiliano duni kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Fedha na Bodi ya Mikopo nchini (HESLB).
Mengine ni HESLB kutoa fedha kwa watu wasiokuwa na sifa pamoja na kile alichokiita utitiri wa vyuo vikuu nchini.
Rais Magufuli alifichua hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kusisitiza kuwa pamoja na changamoto hizo hakuna mwanafunzi wa elimu ya juu mwenye sifa atayekosa mkopo.
Kauli hiyo ya Rais Magufuli imekuja wakati ambao baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa wakiwa katika hali ya sintofahamu baada ya majina yao kutokuwamo kwenye orodha ya kupatiwa mikopo.
Si hilo tu wengine wakilalamikia kuingiziwa fedha pungufu na hivyo hali hiyo kuzua taharuki miongoni mwao.
Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Joyce Ndalichako, wanafunzi waliodahiliwa kwa mwaka huu ni 58,000, kati ya hao waliokidhi vigezo vya kupatiwa mkopo na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ni 25,000.
Taarifa zilizopo waliopatiwa mikopo hadi sasa ni 11,332 na hadi kufikia jana Serikali ilisema imetoa kiasi cha shilingi bilioni 120 kwa ajili hiyo.
Wakati Serikali ikisema hayo, kwa upande wake Mkurugenzi wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana alisisitiza kuwa bajeti waliyonayo ni ya wanafunzi 25,000 tu na kama kutakuwa na wanafunzi wengine wenye sifa wanaohitaji mikopo hawatakuwa na uwezo wa kuwapatia.
Hata hivyo, akizungumzia sintofahamu hiyo, Rais Magufuli alisema: “Wanafunzi nawaomba mtulie fedha zinatolewa kwa awamu kulingana na utaratibu wenu wa kufungua vyuo hivyo naamini hakuna mtu atakayekosa mkopo kama anastahili kupatiwa na yupo kwenye orodha ya bodi ya mikopo,” alisema Rais Magufuli.
AFICHUA MADUDU
Akieleza sababu ya kuwapo kwa malalamiko hayo, Rais Magufuli alikiri  kuwepo kwa changamoto na utaratibu mbovu serikalini ambao umechangia  kucheleweshwa kwa utoaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
Alisema Serikali kwa sasa inapita katika wakati mgumu wa kufanya mabadiliko  wa utaratibu mbovu uliokuwepo ambao ulikuwa unachangia watu wasio na sifa kupata fedha.
“Lazima nikiri hapakuwa na coordination (uratibu), kunatakiwa vyuo vyote viwe na tarehe moja ya kufungua, wapo waliofungua mwezi mzima uliopita wapo waliofungua jana, wapo watakaofungua  keshokutwa.
“Vyuo vikishafungua haraka haraka halafu unawaambia wafanye udahili walipe ada wakati bodi ya mikopo haijatoa fedha na majina ya vijana watakaokopeshwa hiyo ni contradiction (mkanganyiko),” alisema Rais Magufuli.
Alisema katika suala la mikopo kulitakiwa kuwepo na mawasiliano baina ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na bodi ya mikopo ili kuweza kuondoa usumbufu kwa wanafunzi.
Alisema Wizara ya Elimu inapaswa kuanza utaratibu wa kutoa majina na baadaye Wizara ya Fedha wanatoa fedha.
“Hapakuwa na sababu ya kufungua vyuo kabla ya wanafunzi kupata fedha, wanaenda vyuoni wakati hawajapata mkopo, nitoe wito kwa wizara ya elimu na hili nasema kwa dhati lengo la Serikali si kuleta usumbufu kwa wanafunzi.”
Alisema ameshatoa maelekezo kwa wizara ya fedha kutoa Sh bilioni 80 za mwanzo kwa ajili ya mikopo.
“Nawaomba wanafunzi msiwe na haraka, pameshatokea changamoto haitatokea tena, vyuo vitakuwa vinafunguliwa siku ambazo wana uhakika na fedha zimeshaingia katika akaunti.
“Lakini naomba niwe very clear (wazi), Serikali haitatoa fedha kwa wanafunzi wenye uwezo, nimkute mtoto wa Profesa Rwekaza naye nimpe mkopo? Mtoto wa Profesa Ndalichako na yeye nimpe  mkopo? Mtoto wa Kijazi na yeye apate mkopo? Mkopo umelenga kwa ajili ya watoto masikini tu,” alisema.
Alisema wanafunzi wanapaswa kujua kuwa Serikali kwa sasa inapita katika wakati mgumu wa kufanya mabadiliko ya kiutendaji hivyo ni vema wakawa wavumilivu.
“Tunapita katika wakati mgumu wa kufanya mabadiliko kutokana na tabia zilizojijenga na mind set (fikra) huwa ina ugumu wake kuzibadili, kila mahali hewa mabehewa hewa, makontena hewa meli zimeingia bila kujiandikisha hawakulipa kodi, niwaombe viongozi na wanafunzi tunapopitia challenge (changamoto) hii muivumilie Serikali,” alisisitiza Magufuli.
Alisema wakati Serikali inahangaika kutafuta fedha za mikopo wanafunzi wanapaswa wafahamu kuwa wapo  wananchi wenye mahitaji mengine ya kitaifa.
“Wakati unataka kujenga barabara, shule, unahitaji kulipa mishahara wakati huo huo Karagwe wana njaa, wakati huo huo wanahitaji madawa, unataka kutoa elimu bure, halafu wapo watu wanaodhani kuwa unakusanya fedha kwa ajili yao tu.
“Vizuri kuwa unpopular president (rais asiyependwa) lakini utimize yale unayoyaahidi, zinazohitajika zaidi ya Sh bilioni 157, wanafunzi watumie fedha kwa ajili ya kusoma,” alisema.
Rais Magufuli aliitaja changamoto nyingine ya malalamiko ya wanafunzi kuwa imechangiwa na HESLB ambao wanatoa fedha kwa watu wasiokuwa na sifa na kuwaacha wenye vigezo.
“Nasikia bodi ya mikopo nako kuna upendeleo wa kuwapatia mikopo watu wasiostahili, sitaki siku moja niende bodi nichukue orodha ya wanafunzi wote niangalie shule walizosoma na particular walizojaza halafu nikute majina ya watu wasiostahili kupata mkopo.”
Rais Magufuli alisema hashindwi kwenda Bodi ya Mikopo na kujifungia saa 12 kupekua karatasi moja moja ya wanafunzi 25,000 walioorodheshwa kupatiwa mkopo mwaka huu jambo ambalo alisema hataki afike huko.
Alisema changamoto nyingine imechangiwa na uwepo wa utitiri wa vyuo vikuu nchini.
“Utakuta kinafunguliwa chuo kingine Bagamoyo kina wanafunzi 20, bodi mpitie hii mnatoa vibali mno vya kuanzisha vyuo wakati vilivyopo havijajaa na vingine havina walimu, unakuta mwalimu leo yupo Dar es Salaam kesho yupo Mbeya, keshokutwa Moshi,” alisema Rais Magufuli.
Katika hilo alisema haiwezekani kila mahali kuna chuo hadi vichochoroni na kwamba hicho ni kiashiria cha Taifa kupoteza mwelekeo.
“NIT (Chuo cha Usafirishaji) mfano nacho siku hizi Chuo Kikuu! Dereva wangu amesomea pale mimi nasema kwa uwazi siogopi, tunajua Sokoine ni kilimo, Mzumbe cha maofisa utumishi, leo sifahamu hata kama kinafundisha watumishi pale, nalisema hili kwa sababu mimi ni Mtanzania nimefaidika na  matunda ya Uhuru,” alisema Rais Magufuli.
Alibainisha katika bajeti 2015/2016 zilitengwa Sh bilioni 340 kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi 90,000, baada ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani ilitenga Sh bilioni 473 kutokana na makusanyo na kutoa mkopo kwa wanafunzi 124,358.
“Mwaka huu zaidi ya Sh bilioni 487, wanafunzi wengi zaidi watapata mkopo, ninafahamu wanafunzi wanaoendelea wote watapata mkopo pamoja na wanafunzi wapya zaidi ya 25,000,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia aliwataka wafanyakazi wote waliofaidika na mikopo kuanza kulipa madeni yao kwakuwa Serikali inadai Sh trilioni 2.6 katika kundi hilo.
Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha Rais Magufuli, Waziri Ndalichako alisema wanaolalamika kuhusu idadi ya watu kupata mikopo wanapaswa kufanya utafiti kwanza.
“Nimeona baadhi ya vyombo vya habari  vinasema wanafunzi 69,000 wamekosa mkopo, ndugu zangu Watanzania kama hamna data tusipende kuongea, wanafunzi waliodahiliwa ni 58,000 itakuwaje waliokosa mikopo wawe 69,000 kwa hiyo kwa kweli mambo mengine mheshimiwa rais imebidi niyachomeke kwa sababu ni kama kuna  lengo la kutuvunja moyo,” alisema Profesa Ndalichako.
Mbali na hilo, Profesa Ndalichako aliwataka wanafunzi wa vyuo vikuu kutojiingiza katika siasa za kupotosha kazi nzuri inayofanywa na Serikali.
Alisema Serikali katika bajeti yake imetenga Sh bilioni 483 kati ya wanafunzi 119,012 kwa ajili ya elimu ya vyuo vikuu na tayari Sh bilioni 120 zimeshatolewa kwa malipo ya awali kwa wanafunzi wapya 11,332 wa mwaka wa kwanza na wengine 32,997 na Sh bilioni 40 zimeshatolewa kwenye vyuo kwa ajili ya ada.
Kwa mujibu wa Ndalichako, kutokana na vigezo vipya vya mikopo walivyoweka, Wizara yake iko makini katika utoaji wa mikopo hiyo na kwamba haitampa mwanafunzi mwenye uwezo wa kifedha.
Akizungumzia mradi ujenzi wa mabweni 20 yenye ghorofa nne kila moja  unaogharamiwa na Serikali, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema utaweza kuhudumia wanafunzi 3846.
Alisema mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 10 unajengwa na Wakala wa Majengo nchini (TBA) na unatarajia kukamilika Desemba 30, mwaka huu.
Nje ya mradi huo chuo kimetenga zaidi ya Sh bilioni 4.5 zilizotokana na mapato ya ndani ya chuo ikiwamo ya duka Mlimani City kwa ajili ya thamani za ndani kama vitanda na meza za kusomea.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx