WAKATI serikali ikiweka lengo la kukusanya mapato kwa asilimia 100, kauli ya Rais John Magufuli ya kudai risiti bidhaa zinaponunuliwa ilichukua nafasi kubwa katika Semina ya Madiwani wa Manispaa ya Tabora.
Akitoa mada juu ya ukusanyaji wa mapato, mratibu wa semina hiyo, Hamisi Mjanja alisema bila kuwepo na risiti halmashauri haziwezi kupata mapato ya kutosha, kwani yanaweza kuishia mifukoni mwa watu.
Alisema ni wajibu wa madiwani na wakuu wa idara kuhimiza na kutoa elimu kwa wananchi kudai risiti na kutoa risiti wakati wanapofanya biashara yao ili kuziwezesha halmashauri kukusanya mapato kwa asilimia 100.
Hoja hiyo ilionekana kuchukua taswira mpya na kuwavutia waliokuwa kwenye mafunzo hayo wakitoa pongezi kwa Mjanja kwa mada yake yenye kunusuru upotevu wa mapato.
Akizungumzia jinsi madiwani wanavyoweza kuchochea ukusanyaji wa mapato, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Queen Mlozi alisema madiwani wana nafasi kubwa kwa kuwa muda mwingi wapo karibu na wananchi.
Alisema kama madiwani watatambua wajibu wao na kusimamia shughuli zote za maendeleo katika kata zao, halmashauri zitakusanya mapato kwa asilimia kubwa pasipo kuwa na shaka ya upotevu wa mapato.
Mlozi aliongeza kuwa, suala la kupaisha uchumi katika kata zao ni kutoa hamasa kwa wananchi wao kuchangia huduma mbalimbali za kijamii na kuomba risiti wakati wanaponunua bidhaa mbalimbali kutoka madukani na gulioni.