Rais
wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein amesema serikali ipo madhubuti
katika kupembua misaada ambayo wahisani mbalimbali wapo tayari na katika
misaada ambayo itakuwa na masharti magumu kwa sasa serikali haipo
tayari kuipokea kwa manufaa ya wananchi.
Dkt. Shein aliyasema
hayo juzi katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge zilizofanyika
kitaifa katika mkoa wa Simiyu na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali na
taasisi binafsi pamoja na mamia ya wananchi pamoja na watoto wa halaiki
waliopamba shughuli hiyo.
“Serikali
kwa sasa tumejipanga vizuri hatutakubali misaada yenye masharti magumu
na wahisani ambao wanataka kufanya hivyo wakae na misaada yao
tutajitegemea wenyewe” Alisema Dkt. Shein.
Aidha Rais Dkt. Shein aliwataka
watanzania kuendelea kuiunga mkono serikali kwa kuwa imedhamiria
kufanya kazi kwa juhudi zote na kusema kwamba ambao wamezoea kuchukua
rushwa ni bora waache kwa kuwa serikali haitawavumilia.
Mbio za Mwenge mwaka huu zilifikia
tamati baada ya kukimbizwa katika mikoa 31, halmashauri 179 na siku 179
ambapo zimezindua miradi 1,387 yenye thamani ya shilingi bilioni 498.8.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwakani zitazinduliwa mkoani Katavi na kuzimwa mkoani Mjini Magharibi visiwani Zanzibar.