Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Zubeir Kabwe amesema Tanzania haina dikteta uchwara na kudai kuwa ina dikteta mambo leo.
Zitto ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam baada ya msemaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ole Sendeka kusema kuwa nchi haiendeshwi kidekta na kwamba wanaosema hivyo ni wachache waliobanwa kutafuna mali na fedha za nchi.
Zitto amefafanua kuwa dikteta uchwara ni kiashiria cha udikteta na kwamba nchi haina kiongozi wa aina hiyo.
Ameeleza kuwa dikteta mambo leo ni kiongozi anayetaka kutatua kero za wananchi pasipo kutaka kuhojiwa.
“Dikteta mambo leo anawapa mnachotaka ila msihoji vinapatikanaje. Tabia hiyo ipo hapa nchini mfano serikali imenunua ndege pasipo kutaja gharama za manunuzi, inawezekanaje ikawa siri wakati fedha zilizotumika ni kodi za wananchi na si mtu binafsi? “
Ameongeza kuwa “Pia hatuna dikteta kwa sababu siamini kama rais na kundi lake litajinufaisha na mali za watanzania, “
Hata hivyo, Zitto amewaasa viongozi wa upinzani walioshikilia halmashauri za manispaa na miji, kuzifanya manispaa zao kuwa mfano wa kuigwa katika maendeleo na utatuaji wa kero za wananchi badala ya kuilalamikia serikali kuwa haitatui kero za wananchi wake.
“Karibu manispaa 35 zinashikiliwa na upinzani ambao umepewa dhamana na wananchi kuwaletea maendeleo na kwamba wasipo tekeleza ahadi zao hakuna wakumlaumu kwa sababu Rais John Magufuli hawezi sambazia watu huduma za maji, dawa na kadhalika,” amesema.
Vile vile ameshangazwa na kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda cha kuingilia majukumu ya Meya wa jiji hilo
“Mkuu wa mkoa anatenda majukumu ya meya kivipi? Hana mamlaka hayo,wenye jukumu la kusimamia usafi ni manispaa ikiongozwa na meya yeye anaingilia kwa nini? ” amehoji Zitto.