Nape ameyasema hayo alipokuwa akizungumzia taarifa ya Serikali kuyakataa mapendekezo 72 kati ya 227 yaliyotolewa na mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa, likiwemo suala la sheria ya makosa ya mtandao na hali ya kisiasa Zanzibar.
Serikali ilikataa mapendekezo hayo kupitia tamko lililosainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Profesa Sifuni Mchome lililotolewa kwenye mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu wakati wa kupitisha ripoti ya tathmini ya dunia.
Ingawa Nape alisema bado hajaipata taarifa hiyo, aliitaka Marekani ambayo hivi karibuni imekosoa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kile ilichodai kushindwa kulinda utawala wa kidemokrasia, ianze kwa kujinyooshea kidole kabla haijaiangalia Tanzania.
“Kama kuna sheria zimepitishwa hapa na wananchi wanazilalamikia ni sawa, lakini sio Marekani. Wao walienda Iraq, walienda Libya nani amewauliza?” Nape anakaririwa na Mwananchi. “Sheria ya makosa ya Mtandao ya Marekani ni kali kuliko hii ya Tanzania,” aliongeza.
Marekani imekuwa ikiikosoa sheria ya Makosa ya Mtandao tangu ilipoanza kufanya kazi mwaka 2015 na imekuwa ni sehemu ya sababu zilizopelekea kuinyima Tanzania msaada wa karibu shilingi trilioni 1 kupitia MCC.
Katika hatua nyingine, Profesa Mchome alieleza sababu za kutokubali mapendekezo juu ya sheria ya mtandao ni kuwa na kesi zinazoendelea nchini zinazopinga sehemu ya sheria hiyo hivyo wanasubiri ziishe.