test

Jumatatu, 26 Septemba 2016

Wamarekani wasifu, wataka kununua ndege kama za Tanzania



JARIDA mashuhuri duniani la Forbes, limezitaja ndege aina ya Bombardier Dash8 Q400, ambazo tayari Tanzania imezinunua kuwa ni zenye usalama, zinazotumia mafuta kidogo. Limetabiri kuwa zitakuwa nguzo muhimu kwa usafiri wa bei nafuu kwa nchi mbalimbali.

Kwa mujibu wa makala iliyochapishwa na jarida hilo ikiwa na kichwa cha habari “Can Bombardier’s Q400 Save Regional Air Service in the US?”, mwandishi anafafanua faida ya ndege hizo, ikilinganishwa na ndege nyingine zinazofanya usafiri wa ndani nchini Marekani.
“Bombadier ina kasi nzuri na ya kutosheleza mahitaji ya safari za ndani kwa kiwango cha kuwa na faida zaidi kibiashara, ikilinganishwa na ndege nyingine za aina yake kama ATR,” linaandika jarida hilo la Forbes.
Aidha, jarida hilo linataja faida nyingine ya ndege hizo kuwa ni uwezo wa kutumia mafuta kidogo, jambo litakalosaidia kupunguza gharama za usafiri huo wa ndege nchini kwa wasafiri wa ndani. Jarida hilo linafafanua kuwa kiwango kidogo cha mafuta, kinachotumiwa na ndege hizo, kunazifanya kuwa na ufanisi wa asilimia kati ya 48 mpaka 50 zaidi ya ndege nyingine.
Forbes linasisitiza kuwa kutokana na gharama za matengenezo kupanda na gharama nyingine za uendeshaji, ikiwemo mishahara mizuri kwa marubani, kuna uwezekano mkubwa kwa Bombardier kuendeshwa kwa bei rahisi na ikauza tiketi kwa bei rahisi zaidi kuliko ndege nyingine.
“Kwa sasa tunakadiria kuwa ndege aina ya Bombardier, ndizo zitakuwa mbadala na zitashika njia nyingi za ndani (Marekani) kwa kiasi cha asilimia 50 hadi 60 na zitasaidia kurejesha usafiri uliositishwa kutokana na gharama kubwa kwa ndege nyingine katika viwanja takribani 20,” linafafanua jarida hilo.
Akikaririwa katika makala hayo, Mike Arcamone, Rais wa Masuala ya Biashara wa Bombardier anasema wasiwasi wa awali wa abiria kuhusu ndege hizo kutumia mfumo wa turbo, sasa umeondoka kwa kuwa injini na miundo ya kisasa ya ndege hizo, inaifanya isiwe na kelele kama ilivyodhaniwa.
“Wanunuzi wengi wa ndege hizi, wamebaini kuwa hazina kelele na watumiaji wengi wanaamini kuwa zinaweza kuwa mbadala wa ndege nyingine za bei nafuu,” anasema ofisa huyo, kauli inayokubaliwa na wachambuzi wa Forbes.
Tayari Serikali ya Tanzania imeahidi kuleta ndege nyingine ya pili wiki hii, baada ya ile ya kwanza kuwasili nchini wiki iliyopita ukiwa ni mkakati na utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli ya kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Kuwasili kwa ndege hizo, pia kunaonesha Rais Magufuli anavyojitahidi, akiwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake.
Mbali na kuleta ndege hizo, yapo mambo mengi makubwa ambayo Rais Magufuli ameanza kuyatekeleza, aliyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, hatua ambayo imewavutia watu wengi ndani na nje ya nchi.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx