WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesema hadi sasa wizara hiyo haina deni inayodaiwa na walimu nchini na kwamba madeni yaliyokuwepo ya Sh bilioni 22 yalishalipwa.
Profesa Ndalichako alisema hayo juzi jioni wakati akizungumza kwenye kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa hewani moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1).
Akizungumzia madeni ya walimu, alisema serikali inawajali walimu nchini na zipo jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa kuhakikisha madai yao yanahakikiwa na kulipwa ili kuepuka malimbikizo.
Alisema madeni ya walimu yako ya aina mbili; moja ni madeni ya mishahara ambayo wao wizara hawayashughulikii bali yapo chini ya Ofisi ya Rais, Utumishi na kwamba madai aina ya pili ni yale yasiyo na mshahara kama vile likizo, matibabu na mengineyo, ambayo yako chini ya wizara yake na hadi sasa wameshalipa Sh bilioni 22 na hakuna madeni mengine kutoka kwa walimu na kuwataka walimu nchini kama wana madeni mapya kuanzia sasa wayawasilishe wizarani kwa ajili ya kuhakikiwa na kulipwa.
“Wizara tunatambua mchango wa walimu na umuhimu wao kwa upande wetu, hatuna madai yoyote ya walimu yale yanayotuhusu, kwa sababu huwa tuna utaratibu wa kulipa kadri tunavyoyapata na kama yapo kwa sasa wayalete, fedha za kulipa zipo,” alisema Profesa Ndalichako.

