Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amewataka
Watanzania kuwa wazalendo na kutokubali kuamliwa mambo na Marekani ikiwa
ni pamoja na ukosoaji wao juu ya sheria ya makosa ya mtandao.
Nape
ameyasema hayo alipokuwa akizungumzia taarifa ya Serikali kuyakataa
mapendekezo 72 kati ya 227 yaliyotolewa na mataifa wanachama wa Umoja wa
Mataifa, likiwemo suala la sheria ya makosa ya mtandao na hali ya
kisiasa Zanzibar.
Serikali
ilikataa mapendekezo hayo kupitia tamko lililosainiwa na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Sheria na Katiba, Profesa Sifuni Mchome lililotolewa kwenye
mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu wakati wa kupitisha ripoti ya
tathmini ya dunia.
Ingawa
Nape alisema bado hajaipata taarifa hiyo, aliitaka Marekani ambayo hivi
karibuni imekosoa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kile ilichodai
kushindwa kulinda utawala wa kidemokrasia, ianze kwa kujinyooshea kidole
kabla haijaiangalia Tanzania.
“Kama
kuna sheria zimepitishwa hapa na wananchi wanazilalamikia ni sawa,
lakini sio Marekani. Wao walienda Iraq, walienda Libya nani amewauliza?”
Nape anakaririwa na Mwananchi. “Sheria ya makosa ya Mtandao ya Marekani
ni kali kuliko hii ya Tanzania,” aliongeza.
Marekani
imekuwa ikiikosoa sheria ya Makosa ya Mtandao tangu ilipoanza kufanya
kazi mwaka 2015 na imekuwa ni sehemu ya sababu zilizopelekea kuinyima
Tanzania msaada wa karibu shilingi trilioni 1 kupitia MCC.
Katika
hatua nyingine, Profesa Mchome alieleza sababu za kutokubali
mapendekezo juu ya sheria ya mtandao ni kuwa na kesi zinazoendelea
nchini zinazopinga sehemu ya sheria hiyo hivyo wanasubiri ziishe.