Serikali imesema haitawapa kazi wakarandasi nane waliokuwa waliokuwa wakitekeleza miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA), kutokana na kuonesha udhaifu na kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kauli hiyo imetolewa juzi na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani Kagera.
Profesa Muhongo alisema Serikali haiweze kuendelea kufanya kazi na wakandarasi wazembe wasiofikia malengo kwa kuwa wanakwamisha juhudi za Rais Dk. John Magufuli za kutaka kuwaondolea matatizo wananchi walioteseka kwa miaka mingi.
Bila kuwataja wakandarasi na kampunin zao, Profesa Muhongo alisema, tayari Serikali imefanya upembuzi wa wakandarasi waliotimiza wajibu wao wakati wa utekelezaji wa REA awamu ya pili na kubaini wakandarasi nane hawakufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Tunayo majina ya wakandarasi nane ambao kazi zao hazikuturidhisha, walishindwa kufikia malengo yaliyokuwa yamewekwa na hivyo hatutathubutu kuwapa kazi tena katika REA awamu ya tatu, tukiendelea kufanya kazi na watu wa aina hii Serikali haitafikia lengo lake la kuwaondolea wananchi changamoto za kukosa nishati hii ambayo ni muhimu katika uchumi wa wakazi wa vijiji.
“Kama Serikali tuwahakikishie wananchi kwamba vijiji vyote nchini vitakuwa vimepata huduma ya umeme katika kipindi cha miaka mitano kupitia Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), kwani tayari zimetengwa Sh trilioni moja kwa ajili ya shughuli hiyo, fedha nyingi kuliko zilizowahi kutengwa,”alisema.
Profesa Muhongo alisema utekelezaji wa REA awamu ya tatu utakuwa na kasi kubwa na Serikali itahakikisha unakamilika kwa wakati kama ilivyokusudiwa huku akiwatahadharisha wakandarasi watakaopewa mradi huo kufanya kazi kwa bidii.
Katika hatua nyingine, Profesa Muhongo aliwaasa wafanyakazi hao wa Tanesco kujiepusha na vitendo vya rushwa au kutengeneza mazingira yanayoweza kusababisha ufanisi wa kazi kutokuwapo.
Hata hivyo katika kuonyesha dhamira hiyo ya kuepuka rushwa, wafanyakazi hao walikula kiapo mbele ya Profesa Muhongo na kuahidi kwamba hawatajihusisha na vitendo vya rushwa.