test

Jumanne, 13 Septemba 2016

Mitambo ya kupima tetemeko yaibwa



WAKATI taifa likiwa katika majonzi kutokana na vifo 16 vilivyotokana na tetemeko la ardhi na kuacha majeruhi zaidi ya 253 mkoani Kagera wiki iliyopita, siri ya kushindwa kupimwa matetemeko nchini imebainika.
Imeelezwa kuwa vituo vitatu vikubwa vya kupima matetemeko   vimefungwa baada ya kuhujumiwa na vingine vidogo 38 navyo vimefungwa baada ya wafadhili kujitoa.

Hayo yalielezwa  jana na Jiolojia Mwandamizi wa Wakala wa Jiolojia Tanzania, Gabriel Mbogoni alipozungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu.
“Kwa kweli wanajiolojia tunapata changamoto kubwa katika kupima na  kujua iwapo tetemeko litatokea katika eneo fulani na hiyo inatokana na kuhujumiwa  baadhi ya mashine katika vituo vyetu.
“Tulikuwa na vituo zaidi ya 10 vya kupima matetemeko, hivi sasa  vimebaki tisa pekee  na ili kupata uhakika kama kuna tetemeko kwenye eneo fulani lazima uwe na vituo zaidi ya vitatu,” alisema.
Alisema vituo vilivyofungwa baada ya   kuibwa  vilikuwa katika mikoa ya Morogoro, Dodoma (Ntuka) na Arusha  eneo la Longido.
“Ili tuweze kusimika mashine za kupima tetemeko tunahitaji kupata eneo ambalo lina mwamba mgumu.
“Zamani tulikuwa tukitafuta maeneo yenye miamba migumu huko vijijini, tukipata tunawasiliana na viongozi wa kijiji na tunaweka walinzi wa kulinda mashine hizo.
“Lakini zimeibwa hali iliyosababisha kufungwa   vituo hivyo…tulipeleka kesi mahakamani mwisho tukaona ni vema sasa tuanze kuzifunga mashine hizo katika maeneo ya magereza kwa usalama wake isipokuwa kile cha Mtwara na Dodoma,” alisema.
Alisema wezi hao, wamekuwa wakiiba mashine hizo wakidhani  wanaweza kunufaika, wakizifananisha na madini.
“Wengi wanadhani zinamilikiwa na Wizara ya Nishati na Madini kwamba wakiziiba watauza wapate faida.  Unajua mashine hizi zipo kama sanduku, wanapoziiba huwa hawawezi kuziuza popote kwa sababu zinatambulika,” alisema.
Mbogoni alisema vituo vikubwa vilivyobakia vipo katika mikoa ya  Mtwara, Dodoma, Geita, Arusha, Babati, Singida, Mbeya na Manyara.
Akizungumzia  vituo vidogo 38 vilivyofungwa, alisema hiyo ilitokana na kumalizika  mradi wa kupima matetemeko uliokuwa ukifanywa na wakala huo kwa kushirikiana na Chuo cha Pennyslvania State cha Marekani.
“Siwezi kutaja tumepata hasara kiasi gani kwa sababu sijui mashine hizo zilinunuliwa kiasi gani na sasa zinauzwa kiasi gani. Huwa tunazipata kutoka  kwa ufadhili wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali.
“Awamu ya kwanza wa mradi ulianza 2007 hadi 2008 halafu ukaanza tena 2013 hadi April 2015 ambako uliisha,” alisema.
Mbogoni alisema matetemeko mengine madogo yataendelea kutokea kwa muda.
“Ni hali ya kawaida linapotokea tetemeko kubwa huwa baadaye yanatokea mengine madogo madogo, yanaweza yakadumu hata kwa wiki au hadi miezi minne.
“Hii ni kwa sababu ile nguvu ya mgandamizo inayotokea ambayo husababisha miamba kumeguka huwa bado haijaisha na ndiyo maana tetemeko huendelea kutokea,” alisema.
Juzi, tetemeko kubwa lilitokea katika maeneo ya Kanda ya Ziwa hususan mkoani  Kagera lilisababisha zaidi ya vifo 15 huku likiacha majeruhi zaidi ya 253.
Tetemeko hilo limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 kupata nyufa, yakiwamo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx