Idadi
ya watu wanaokamatwa kwa tuhuma za kumkashfu Rais John Magufuli kupitia
mitandao ya kijamii imezidi kuongezeka baada ya polisi kumkamata
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa (Muce), Dk Oscar
Magava (48).
Dk
Magava amekuwa mtu wa kumi kukamatwa na polisi katika kampeni za jeshi
hilo kudhibiti uhalifu chini ya sheria ya uhalifu wa mtandaoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi alisema Dk Magava alikamatwa akiwa Sumbawanga na alirudishwa mkoani Iringa.
Mjengi
alisema Septemba 15, mwaka huu walipata taarifa kuwa mhadhiri huyo
anatumia mitandao ya kijamii kumkashfu Rais. Alisema waliamua kumsaka na
walipopata taarifa kuwa Dk Magava amekwenda Sumbawanga waliwasiliana na
polisi wa huko wakamkamata na kumrudisha Iringa.
Hata
hivyo, Kamanda Mjengi hakuyataja maneno aliyotumia Dk Magava kumkashfu
Rais kwa madai kuwa bado wanaendelea na uchunguzi na kwamba ukikamilika
atafikishwa mahakamani.
Kamanda
Mjengi aliwatahadharisha wananchi kuwa makini na matumizi ya mitandao
ya kijamii kwa kuitumia kwa ajili ya maendeleo na si kutukana wala
kukashfu viongozi au watu wengine.
Watu mbalimbali wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kumkashifu Rais au jeshi la polisi.