Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema jana kuwa, haijapokea
mabadiliko yoyote ya uongozi kutoka katika chama hicho, hivyo
wanaendelea kumtambua Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa chama
hicho.
Aidha, ofisi hiyo ya msajili wa vyama vya siasa imesema msimamo wake
upo pale pale kwamba Lipumba ni Mwenyekiti halali wa CUF kwa mujibu wa
Katiba ya chama hicho mpaka hapo itakapoelezwa tofauti kwa kusimamia
sheria za vyama vya siasa na Katiba ya chama hicho.
Hivi karibuni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa msimamo wa
msajili ni kwamba bado Lipumba ni Mwenyekiti halali wa CUF na wanachama
wote waliofukuzwa uanachama na kikao cha Baraza Kuu la Uongozi cha
Agosti 28 mwaka huu ni halali.
Alitoa angalizo kuwa, kamati iliyoundwa kuongoza chama na viongozi
walioteuliwa si halali na kwa kuwa kifungu cha 8B (2) cha Sheria ya
Vyama vya Siasa Sura ya 258 kinaeleza kuwa mtu yeyote ambaye si kiongozi
wa chama haruhusiwi kufanya kazi za chama kama viongozi, ofisi yake
haiwatambui viongozi hao.