Mvutano
wa uenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) unatajwa kuwa ni tishio kubwa
kwa umoja wa vyama vya siasa wa Ukawa ambao chama hicho ni sehemu ya
nguzo kuu, hali iliyoibua maoni tofauti kati ya viongozi wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Makamu
Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Profesa Abdallah Safari, amekiri kuwa
mgogoro huo utaiathiri Ukawa ambayo Profesa Ibrahim Lipumba
anayeupigania uenyekiti wa CUF alikuwa mmoja kati ya waasisi wake lakini
aliutosa baadae akipinga uwepo wa Edward Lowassa.
“Spirit
ya Ukawa ni umoja uliojitokeza baada ya kuaminiwa na Watanzania. Sasa
hali hii inaathiri kwa kiasi fulani,” Alisema Profesa Safari.
Profesa Safari aliifananisha hali hiyo na kuwa na golikiba mzuri wa timu ya mpira wa miguu ambaye ni mlemavu wa miguu.
Akizungumzia
barua ya Msajili wa vyama vya siasa iliyoeleza kumtambua Profesa
Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF, Profesa Safari alisema kuwa
msajili anajua ukweli kuwa ushauri wake hauwezi kuchukuliwa kama uamuzi
wa mwisho kumrudisha Profesa Lipumba kwenye nafasi ya uenyekiti wa chama
hicho lakini aliamua tu ‘kuvuruga’.
Alisema kuwa ili kupata uamuzi wenye mamlaka kisheria juu ya mgogoro huo, Profesa Lipumba anapaswa kwenda Mahakamani na sio CUF.
Hata
hivyo, Mbunge wa Tarime vijijini (Chadema), John Heche alitofautiana na
mtazamo wa Profesa Safari kuhusu mgogoro huo wa CUF akidai kuwa Profesa
Lipumba hawezi kuuyumbisha umoja huo.
“Ukawa
haiwezi kuyumbishwa na Lipumba, Ukawa ilianzishwa na wabunge [wa bunge
la katiba]na sio ushawishi wa Liumba,” alisema Heche.
Juzi,
Profesa Lipumba aliingia kwa nguvu ndani ya ofisi za makao makuu ya CUF
zilizoko Buguruni jijini Dar es Salaam baada ya wafuasi wake kuvunja
mlango na kuwapiga walinzi waliokuwa zamu.
Lipumba
ameendelea kueleza kuwa yeye ndiye mwenyekiti halali wa chama hicho
huku akipinga maamuzi ya kusimamishwa uanachama yaliyotolewa na Baraza
Kuu la chama hicho akidai kikao kilichofikia maamuzi hayo hakikuwa
halali.
Kufuatia
tukio la kuvunja ofisi na kuingia ofisini kwa nguvu, Naibu Katibu Mkuu
wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui alisema kuwa wamemuandikia Lipumba barua ya
kumtaka ajitetee mbele ya Baraza Kuu la chama hicho kwanini
asichukuliwe hatua kwani kitendo hicho ni kinyume cha katiba ya chama.
Hata hivyo, Lipumba amesema hajaipata barua hiyo na wala haitambui.