Vyanzo vya ndani kutoka katika mahakama hiyo vimeeleza kuwa, tayari mahakama imetoa samansi ya kumuita mtuhumiwa ili kesi hiyo ianze kusikilizwa.
“Hivi mna habari kuwa kesi ya Lulu itaanza kusikilizwa siku ya Ijumaa Agosti 26 na inafanywa kuwa usiri mkubwa sidhani kama waandishi wa habari
watapata nafasi ya kuripoti, hata samansi zimetumwa kimyakimya kwa wahusika,” kilisema chanzo hicho kutoka mahakamani.
Chanzo hicho kilizidi kutiririka kuwa, kadiri kesi hiyo itakavyoanza kusikilizwa, Lulu atatakiwa kujibu tuhuma zinazomkabili ambapo mwigizaji huyo anadaiwa kutenda kosa hilo mnamo Aprili 7, 2012.
“Kwa kuwa ndiyo kesi itaanza kusikilizwa, Lulu atatakiwa kujibu kama ni kweli ametenda kosa hilo au la na hapo
baadaye ndipo majaji watakapotoa hukumu,” kilisema chanzo hicho.
Jitihada za kumpata Lulu ili aweze kuzungumzia kesi hiyo inayomkabili na namna alivyoipokea samansi ya mahakama hazikuzaa matunda kufuatia simu yake kutokuwa hewani hadi tunakwenda mitamboni.
Aidha, mwanahabari wetu alimvutia waya, mama mzazi wa
marehemu Kanumba, Flora Mtegoa ili kujua kama ana taarifa za kesi hiyo kuanza kusikilizwa ambapo alipopatikana alikiri kesi hiyo kuanza kusikilizwa.
“Nimesikia kweli inaanza kusikilizwa Ijumaa hii (Agosti 26), mimi sina la kusema nafurahi tu ili kesi hiyo iishe na ninaamini mahakama itatenda haki, nipo tayari kupokea jibu lolote lile,” alisema mama Kanumba.
Awali, kesi hiyo ilikuwa ni mauaji na ilianza kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kisha ikahamia Mahakama Kuu ambapo baada ya mabishano baina ya mawakili wa utetezi na mwendesha mashtaka wa serikali, shtaka hilo lilibadilishwa na kuwa la mauaji ya bila kukusudia