test

Jumatatu, 15 Agosti 2016

RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 31



 Mtunzi:ENEA FAIDY


...Doreen alimsikiliza kwa Umakini mama Pamela ili ajue ni swali gani analotaka kuuliza. Mama Pamela alikaa vyema kisha akakohoa kidogo na kumtazama Kwa makini Doreen.
"Niulize Tu mama" alisema Doreen.

"Hivi ni kitu gani unapenda nikufanyie ili moyo wako ufurahi? Maana nimependa sana heshima na adabu uliyojaaliwa." Alisema mama Pamela.


"Kiukweli mama Mimi napenda sana unitafutie shule.. Ili niweze kusoma na kufikia malengo yangu" alisema Doreen.
"Shule tu? Wala usijali wiki ijayo nitakuwa tayari nimetafuta shule kwa ajili yako.."


"Nitafurahi sana mama..."
"Unapenda shule ya kutwa au bweni?"
"Yoyote tu itanifaa" alisema Doreen.
Suala lile lilimfurahisha sana Doreen, aliendelea kuishi kwa kunyenyekea sana ndani ya nyumba ile, lakini katika ulimwengu mwingine alikuwa ni mtu jeuri na katili kwa familia ile. Kila Mara aliliwinda sana titi la Pamela, alitamani kulipata kwa udi na uvumba lakini kwa bahati mbaya ilikuwa vigumu kulipata. Alitumia kila namna lakini bado hakuelewa sababu ya kushindwa kulipata titi la Pamela.

Hasira zilimuwaka sana Doreen pale alipoingia chumbani kwa Pamela usiku na kutaka kumkata titi lake. Alikuta Pamela amelala usingizi mzito sana, akampulizia dawa ili usingizi ule uzidi kuwa mzito zaidi kisha akamsogelea taratibu akiwa ameshikilia panga Kali lililofungwa kaniki nyeusi na nyekundu. 


Doreen alitamka maneno ambayo aliyajua mwenyewe kisha akamfunua shuka Pamela na kusogeza kisu chake karibu na titi la Pamela. Hakuwa na hofu kama kazi yake haitofanikiwa kwani alikuwa anajiamini na alikiamini kile alichokifanya. Lakini kwa bahati mbaya sana kila alipotaka kumgusa Pamela na upanga ule, Doreen hakuona chochote kitandani pale. Alijaribu tena na tena lakini bado hali ikaendelea kuwa vile vile. Doreen alikasirika sana, akatupa chini upanga ule mlio wake ukamshtua Pamela usingizini.

Doreen alishtuka sana baada ya Pamela kushtuka usingizini,  akakimbia haraka na kujibanza kwenye kona moja ya chumba kile kisha akatamka maneno Fulani ya kichawi halafu akatulia kimya. 


Pamela aliangaza macho huku na kule chumbani mle lakini hakuona kitu, akainuka kitandani na kuwasha taa kisha akaangalia kila sehemu ya chumba kile lakini hakuona chochote. Akatoka na kwenda msalani, alipokuwa anajisaidia haja ndogo akahisi kuna mtu anamfuata nyuma yake Pamela alishtuka na kuogopa sana kisha akakumbuka jambo muhimu la kufanya kama alivyoambiwa na baba yake. Pamela akasali kwa sauti ya chini na kwa imani kubwa sana kisha akajisaidia na kurudi kitandani, akalala bila kuzima taa.
Doreen alikasirika sana baada ya kumkosa Pamela kwa Mara nyingine. Akaamua kurudi chumbani kwake kupitia  kona ile ile aliyokuwa amejibanza.

Doreen alitokea chumbani kwake akiwa na hasira sana. Alijituliza kimya akiwa amekaa chini sakafuni huku akiwa ameshika tunguli na hirizi mkononi mwake.  Aliamua kuita mizimu ya kwao ili iweze kumsaidia katika hali ngumu aliyonayo.


Ndani ya sekunde chache alitokea mwanamke mmoja Mzee sana. Kichwa chake kilikuwa kimejaa mvi lakini hakuvaa nguo yoyote isipokuwa kaniki nyeusi aliyovaa kiunoni pamoja na shanga nyingi sana alizokuwa amevaa kiunoni mwake na shingoni. USO wake ulikuwa na makunyanzi mengi sana yaliyokuwa yametawaliwa na vitu kama unga unga mweupe. Alipotua tu chumbani kwa Doreen, nyumba nzima ilitikisika kwani alikuwa ni mtu mkubwa sana katika himaya ya uchawi ya akina Doreen.


"Karibu! Karibu! Mama mtukufu! Mkuu wa wachawi wote! Mwenye nguvu kuliko wote duniani!"  Doreen alimkaribisha mgeni wake yule kwa heshima kubwa sana. Yule bibi hakutoa sauti yoyote zaidi ya Kuitikia kwa kichwa tu huku akimsogelea Doreen kwa kutumia makalio yake.


"Doreen! Tangu tumekutuma huku duniani hujawahi kuniita isipokuwa Leo.. Najua una jambo zito linalokusumbua" 
"Ndio! Ndio! Mtukufu"
"Sasa inabidi tutoke humu maana si mahali sahihi"
"Sina pingamizi Bi Tatile! Kipenzi cha wachawi wote" yule Bibi alimshika mkono Doreen kisha taratibu kwa kutumia makalio yao wakasogelea kona ya kushoto kwao. Kisha wakatoweka ndani ya jumba lile. Lakini kitandani kwa Doreen waliacha mwili wa Doreen pekee na hata kama angeamshwa kwa kipindi kile basi asingeweza kuamka .

Safari ya wawili wale kwa kutumia usafiri wa ungo huku dereva akiwa Bi Tatile iliwafikisha mpaka eneo la makaburini ambapo walitua na wakaketi hapo kisha wakaendelea na kikao chao kifupi kilichotokea kwa dharula.

"Sema mjukuu wangu.. Mimi ndo Tatile binti Matatila mwenye uwezo wa kubadili nyasi za kijani zikawa nyeupe.."
"Mtukufu lile suala la kupata titi naona linakuwa gumu sana kwangu.. Nimekamilisha kila kitu lakini bado hilo tu.. Tafadhali naomba unisaidie kwa hili..."


"Ha ha ha hah Doreen wewe una uwezo mkubwa sana wa kukamilisha hilo.. Unaweza ukafanya hivyo haraka sana ila kuna jambo moja tu! Unatakiwa ufanye."
"Jambo gani mtukufu? Niambie tu maana nimechoka kuhangaika" alisema Doreen.


                                        ****

Majira ya saa kumi na moja jioni Dada wa Mama Eddy aliwasili nyumbani kwa Mr Aloyce. Alipokelewa vizuri sana na Bwana Aloyce pamoja na Eddy lakini ilikuwa tofauti sana kwa mama Eddy kwani alimkaribisha Dada yake kama vile alimkaribisha adui yake ndani ya nyumba. Suala hilo liliibua maswali mengi sana kwa Mr Aloyce pamoja na mgeni wao.


"Mama Eddy.. Nakuomba chumbani Mara moja..." Alisema Baba Eddy kisha akaingia chumbani. Mama Eddy alimfuata mumewe ili amsikilize kile anachotaka kumweleza.
"Mke wangu... Mbona unaniabisha kwa shemeji yangu?"
"Kivipi?"
"Dada yako amekuja lakini unamsalimia kama hutaki vile.. kwanini?"  Aliuliza baba Eddy kwa mshangao.


"Nimejisikia tu.."
"Hapana mke wangu usiwe hivyo... Nakuomba basi onesha kumjali mgeni tena nduguyo wa damu.."
"Siwezi kumjali mchawi mkubwa yule..." Alisema mama Eddy akiwa anajishumburua midomo yake kwa dharau.
"Unasemaje? Dada yako mchawi kivipi?"
"Amemroga mwanangu..."


"Umejuaje au nawewe mchawi? Maana haiwezekani umtuhumu mwenzio mchawi wakati huna uhakika?" Alisema Baba Eddy kwa hamaki. Hakutaka kuamini kile alichokisa mkewe.
"Leo hii unaniambia mimi mchawi? OK sawa... " alisema Mama Eddy na kwenda sebuleni kwa hasira.


Alisimama wima akiwa ameshika mkono kiunoni huku akimtazama dada yake kwa dharau.
Dada yake alipigwa na butwaa sana, alibaki anamshangaa mdogo wake kwa vitendo vya dharau anavyomfanyia.
"Wewe!" Alisema Mama Eddy.
"Naomba utoke kwenye nyumba yangu.. Ulichomfanyia Eddy kinatosha..."
"Mimi?"


"Kumbe naongea na nani kama sio wewe mpumbavu..."  Alisema Mama Eddy akidhihirisha chuki kubwa aliyonayo moyoni mwake. Eddy alimtazama mama yake kwa mshangao sana akiwa haelewi sababu ya mama yake kumfanyia unyama ule dada yake wa damu. Hakuna aliyefahamu ukweli kuwa yule hakuwa mama Eddy halisi.


"Mama... Mama mkubwa amekosa nini?"
"Hebu kelele huko na wewe.. Hujui kama huyu ndo aliyekuroga?"
"Sio huyu mama..." Eddy alimtetea.
"Hebu ondoka hapa.. Kwanza hayakuhusu.." Alifoka Mama Eddy.
"Sasa na mimi naondoka na mamkubwa.. Sibaki hapa?" Alisema Eddy.
Wakati huo Mr Aloyce alifika sebuleni pale na kuanza kumuomba msamaha mgeni yule asiye na hatia....

ITAENDELEA.....

Usikose kufuatilia sehemu inayofuata kupitia jungukuuleo.blogspot.com

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx