RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.John Pombe Magufuli ametoa ubani wa Sh milioni 10 kwa familia za askari wanne waliouawa katika shambulio la ujambazi Mbande wilayani Temeke mkoani Dar es Salaaam, huku akiwataka askari kutokuvunjika moyo katika utendaji wao wa kazi kutokana na mauaji ya wenzao, bali walitumie kama kigezo cha kufanya kazi kwa bidii.
Aidha, Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Ernest Mangu na wanafamilia wa askari wote waliopoteza maisha.
Askari watatu kati ya wanne waliofariki katika shambulio hilo la Jumanne usiku katika eneo la benki ya CRDB Mbande, Dar es Salaam ambalo watu wenye silaha waliwavamia wakiwa kazini na kuwaua na kupora bunduki mbili aina ya SMG na risasi 60, waliagwa jana katika Viwanja vya Polisi Barabara ya Kilwa.
Akizungumza wakati wa kuaga miili hiyo katika shughuli iliyoongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, IGP Mangu alisema baada ya tukio hilo kutokea, aliwasiliana na Rais Magufuli ambaye alionesha kusikitishwa sana na tukio hilo na kumpa pole yeye, askari pamoja na familia za marehemu.
Miili ya askari walioagwa jana ni Koplo Yahaya Malima aliyesafirishwa kwenda kuzikwa kijiji cha Kibuta, wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Tito Mapunda aliyesafirishwa kwenda kijiji cha Migoli, wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa na Gaston Lupanga aliyesafirishwa kwenda mjini Songea mkoani Ruvuma kwa maziko.
Askari mwingine Koplo Khatib Ame Pandu alisafirishwa Jumatano jioni kwenda kwao Zanzibar ambako maziko yalifanyika siku hiyo hiyo usiku.
Viongozi mbalimbali wa serikali walipata fursa ya kutoa salamu za rambirambi katika msiba huo, na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliamuru wale wote waliofanya uhalifu huo pamoja na wale wanaofanya vitendo vya uhalifu jijini Dar es Salaam kushughulikiwa ipasavyo.
“Katika hili ninaomba wale wa haki za binadamu wanisamehe, kitendo hiki si cha kuvumilika hata kidogo kwa kuona wale ambao wamekula kiapo kutulinda sisi, leo sisi tunakwenda kuwaua wao halafu tunyamaze, mimi nasema hapa hadharani …Afande Sirro twanga tu yeyote mtakayekutana naye msituni,” alisema Makonda.
Makonda alisema kazi ya amani ya vyombo vya ulinzi ni kubwa hivyo ipo haja ya kuangaliwa upya kwa taratibu na sheria kuona ni namna gani askari kama hao wanaopoteza maishawakiwa bado vijana wadogo kuwajengea hata nyumba ili kuwapa faraja wale wanaowaacha nyuma yao.
Naye Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Sirro alisema kitendo walichofanya wahalifu hao kuua askari ni sawa na kuwasha moto hivyo na wao watajibu mapigo na kuhakikisha wahalifu hao wanapatikana.
“Wameuwasha moto na sisi tutauwasha moto kwelikweli na katika hili tutaomba watu wa Tume za Haki za Binadamu kutosimama upande wowote,” alisema Sirro.
Aidha, Waziri Mwigulu aliagiza Jeshi la Polisi kuendelea bila kukoma kuwasaka majambazi na wahalifu wote na kuhakikisha wanakamata waliofanya tukio hilo.
Mwigulu pia ameagiza viongozi wa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wizara yake kuangalia upya sheria na kuona namna bora ya kuwasaidia askari kuwa na bima za maisha, huku akiwataka kuhakikisha wanaharakisha mafao kwa familia za marehemu yanaandaliwa mapema.