Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH) inatarajia kuanza kutumia mitandao ya simu,
kadi maalimu na kadi za benki kwa ajili ya kulipia huduma za matibabu
ili kudhibiti changamoto za upotevu wa fedha na wizi katika ukusanyaji
wa mapato ya hospitali hiyo.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa
Umma na Huduma kwa Wateja, Bw Aminiel Eligaesha, hospitali hiyo imelenga
pia kuimarisha njia za ukusanyaji mapato ili kuboresha huduma za
matibabu na kuboresha maslahi kwa wafanyakazi.
Amesema
mpango wa kutumia njia za kieletroniki umelenga kukusanya mapato zaidi
ili kuiwezesha hospitali hiyo kukabiliana na changamoto mbalimbali za
uendeshaji na kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
Lengo
la hospitali hiyo ni kuongeza mapato na kupunguza matumizi na
kutengeneza mazingira ya kujiendesha na kutoa huduma bora kwa wagonjwa
mbalimbali nchini.
“Hospitali
imelenga kuboresha wadi za kulaza wagonjwa wanaohitaji huduma na malazi
binafsi, kuhakikisha wagonjwa wanachangia huduma za matibabu na
kuboresha mfumo wa kuandaa hati za madai kwa kampuni na mifuko ya Taifa
ya bima ya afya."
Taarifa
hiyo imeeleza kwamba hospitali hiyo imedhamiria pia kutoa motisha kwa
wafanyakazi wengine ili kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi.
Katika
hatua nyingine, hospitali hiyo imeweka mikakati ya kupunguza gharama za
kununua dawa na vifaa tiba kutoka viwandani (Manufacturers) moja kwa
moja.
“Kwa
mfano, baada ya kupata kibali kutoka TFDA, Hospitali imenunua dawa za
figo (immunosuppressant) kutoka India kwa Sh 226 milioni wakati hapa
nchini zingegharimu Sh 500 milioni,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Pia,
hospitali hiyo imeagiza nyuzi za kushonea wagonjwa (sutures) kutoka
kiwandani (Ethicon) kwa gharama ya Sh 321 milioni wakati zingegharimu Sh
668 milioni endapo zingenunuliwa nchini.
Katika
taarifa hiyo imebainisha kuwa hospitali hiyo imeweza kupunguza gharama
za uchujaji wa damu (dialysis) kutoka wastani wa Sh 250,000 kwa kila
zamu (session) hadi kufikia Sh171,000.