Serikali
ya Marekani, kupitia shirika lake la Misaada ya Maendeleo USAID,
imeipatia Tanzania msaada wa dola Milioni 407 sawa na zaidi ya shilingi
Bilioni 895 zitakazotumika kwaajili ya kuendeleza sekta za Kilimo, Afya,
Nishati ya Umeme, Elimu na Utawala Bora, katika kipindi cha miaka
mitano ijayo kuanzia mwaka 2016/2020.
Hati
za makubaliano hayo zimetiwa saini Jijini Dar es salaam, kati ya
Mkurugenzi wa Shirika la USAID, Bi. Sharon Cromer, na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile.
Msaada
huo ni sehemu ya dola milioni 800, sawa na zaidi ya shilingi trilion
1.76 ambazo serikali ya Marekani kupitia USAID, imepanga kuipatia
Tanzania ili kufanikisha Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa katika
kipindi cha miaka mitano ijayo, wenye lengo la kuiwezesha Tanzania
kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025.
Kiasi
hicho cha fedha kitatumika na serikali ya Tanzania kupitia mfuko mkuu
moja kwa moja wakati kiasi kingine kitatumiwa na Taasisi zisizokuwa za
kiserikali zinazofanya shughuli zake hapa nchini kufanikisha malengo ya
msaada huo.
Miradi
iliyopewa kipaumbele ni pamoja na kupambana na UKIMWI na kifua kikuu,
uzazi wa mpango, kupunguza vifo vya mama na mtoto, kukuza utawala wa
kidemokrasia, usimamizi wa rasilimali za taifa, na kuwekeza kwenye sekta
ya umeme ili kuimarisha sekta ya viwanda na uzalishaji mali.