POLISI
mkoani Kilimanjaro inawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za kumuua
kwa kukusudia mwanamke Neema Ndewera (65), kwa kumchoma kisu shingoni
na sikio la kulia.
Akitoa
taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Willbrod
Mutafungwa, watuhumiwa hao walifanya tukio hilo la kinyama Julai 10,
mwaka huu ambapo baada ya tukio hilo walifukia mwili wa marehemu kwenye
shimo la choo cha nje ya nyumba yake.
Alisema
Ndewera alikuwa akiishi peke yake katika kata ya Mbokomu, ambako Juni
mwaka huu aliaga anasafiri kwenda Arusha kuwaona watoto wake, ambapo
alimuomba jirani yake Michael John kuwa mwangalizi wa mifugo yake ambayo
ni mbuzi wawili, ng’ombe mmoja na kuku.
Alisema
mwanzoni mwa Julai, alirudi nyumbani kwake na kukuta mbuzi na kuku
wameuzwa, hali iliyomlazimu kumuuliza John kuhusu suala hilo ambalo
hakupewa majibu ya kuridhisha.
Mutafungwa
alisema kutokana na hali hiyo Julai 10, John akishirikiana na
watuhumiwa wenzake, wote kwa pamoja walimuua Ndewera ili asiwashtaki kwa
wizi wa mifugo.
Alisema
baada ya tukio hilo watuhumiwa hao waliuza ng’ombe aliyebaki kwa Sh
400,000 kisha kugawana fedha, ambapo walidanganya kuwa Ndewera anaumwa
na amesafiri kwenda Dar es Salaam kwa mtoto wake kwa matibabu.
Alisema
Agosti 12, Polisi ilipata taarifa hizo kutoka kwa raia wema, ambapo
walifika eneo la tukio na kuukuta mwili wa marehemu ukiwa umefunikwa
kwenye shimo la choo ukiwa na kisu shingoni, ambapo uchunguzi ulifanywa
na madaktari na kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu.
Kamanda
aliwataja watuhumiwa wa tukio hilo ni John (24) fundi ujenzi, Nevance
Reginald (46), Mussa Issa (23), Fausta Naftari (29) na Magreth John
(53), wote wanne wakijishughulisha na kilimo.