ALIYEKUWA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson
Maimu na maofisa wengine saba waandamizi, wamepandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na
mashitaka 27 yakiwamo ya matumizi mabaya ya ofisi na kusababisha hasara
ya zaidi ya Sh bilioni 1.2.
Washitakiwa
wengine ni Mkurugenzi wa Huduma za Kibiashara, Avelin Momburi, Meneja
wa Fedha na Uhasibu, Benamini Mwakatumbula, Meneja wa Bajeti na Milki,
Joseph Makani, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima na Mkurugenzi wa
Sheria, Sabina Raymond.
Wengine
ni Xavery Kayombo ambaye wadhifa wake haukutajwa, na Astery Ndefe
ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers Company
Limited. Washitakiwa hao pia wanakabiliwa na mashitaka yanayohusu
kutumia nyaraka zenye kusudio la kudanganya na kula njama za kutenda
kosa.
Mbele
ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage, washitakiwa hao hawakutakiwa
kujibu lolote dhidi ya mashitaka hayo kwa sababu wanashitakiwa chini ya
Sheria ya Uhujumu Uchumi. Wote waliamuriwa kurejeshwa mahabusu hadi
Agosti 31, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.
Uchunguzi
wa kesi hiyo kwa mujibu wa waendesha mashitaka, wanaoongozwa na
Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Awamu Mbangwa haujakamilika.
Hakimu
alisema kwamba suala la dhamana litaamuriwa na Mahakama Kuu, kwa kuwa
kiwango cha fedha katika kesi hiyo kinazidi Sh milioni 10.
Lakini
alisema atatoa uamuzi kuhusu dhamana kwa washitakiwa Mobuli na Makani
kesho kwa sababu ya hoja kwamba wawili hao hawakabiliwi na mashitaka ya
uhujumu uchumi, kama washitakiwa wengine.
Jopo la waendesha mashitaka linawajumuisha pia Leonard Swai, Janeth Machuria, Joseph Kiula na Fatma Waziri.
Waendesha
mashitaka walidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2010 na
2015, wakiwa watumishi wa umma, Maimu na Mwakatumbula walitumia vibaya
madaraka yao kwa kuidhinisha kwa Kampuni ya Gotham International Limited
malipo ya Dola za Marekani milioni 5.175 pamoja na Sh milioni sita.