Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) limemteua Julius Mtatiro kuwa mwenyekiti wa kamati ya muda ya uongozi hadi utakapoitishwa mkutano mkuu maalumu mwingine baada ya ule wa awali kuvunjika.
Mtatiro amekubali uteuzi huo na kwamba hawezi kukwepa majukumu hayo muhimu.
Baraza hilo lililoketi katika kikao chake cha dharura juzi Jumapili mjini Unguja, liliamua pia kusitisha uanachama wa baadhi ya watendaji wake waandamizi, kutoa karipio kali na kuwafukuza baadhi yao.
Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Vuga kilihudhuriwa na wajumbe 47 kati ya 60 na kiliongozwa na Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali.
Akitangaza maazimio ya kikao hicho jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema katika kutekeleza jukumu hilo, Mtatiro atasaidiana na Katani Mohamed Katani na Severina Mwijage.
“Maamuzi hayo ni kwa mujibu wa katiba ya CUF kifungu Na.101 na 118, vinavyolipa mamlaka baraza kutekeleza hatua hiyo.”
Mazrui alisema baraza hilo lilimteua John Bashange kukaimu nafsi ya naibu katibu mkuu wa CUF – Tanzania Bara na Mbaralah Maharangande kukaimu nafasi ya naibu mkurugenzi wa habari, uenezi na uhusiano kwa umma.
Nafasi zilizojazwa ziliachwa wazi na Profesa Ibrahim Lipumba, Magdalena Sakaya na Abdul Kambaya ambao baraza hilo la dharura lilitangaza kuwasitisha uongozi na uanachama wao.
“Hatua ya kuitisha baraza la dharura sambamba na maamuzi hayo ilikuja baada ya kushindwa kupata uongozi wa juu wa chama kufuatia kuvunjika na kushindwa kukamilika kwa mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi wa Agosti 21 uliofanyika jijini Dar es Salaam,”alisema.
Alisema kuwa baraza liliamua kusitisha uanachama wa Sakaya kwa kushindwa kutekeleza kifungu cha katiba ya CUF, Na. 122 na kwamba licha ya barua aliyotumiwa kumtaka ahudhurie kikao hicho, hakufika bila ya taarifa yoyote ya msingi.
Mazrui alisema katika baraza hilo, ilielezwa kuwa Sakaya alidai kuzuiliwa na wazee wa CUF wa Dar es Salaam kwa madai kuwa hicho hakikuwa kikao halali.
Wengine ambao uanachama wao umesitishwa ni Ashura Mustafa, Mohamed Mnyaa, Kapasha Kapasha, Haroub Shaim, Omar Masoud na Thomas Malima.
Baraza hilo la CUF lilitangaza kumfukuza uanachama wa chama hicho, Shashu Lugeye, baada ya kumsikiliza na kutoridhishwa na maelezo yake.
Wanachama waliopewa karipio kali ni Rukia Kassim Mohamed na Othman Mohamed.
“Chama kimechukua maamuzi haya kuonyesha dhamira ya dhati na matumaini ya umma wa Watanzania kwamba CUF ndiyo pekee iliyobeba dhana ya mabadiliko,” alisema Mazrui.
Taarifa kutoka ndani ya Baraza hilo ziliarifu sababu tatu za kuchukua hatua hiyo kuwa ni hasara ya Sh600 milioni kiliyoingia kwa mkutano uliovunjika; njama ovu zilizodaiwa kutekelezwa na baadhi ya watendaji wao; na jaribio la kuchafua taswira ya chama hicho.
Mazrui alisema mkutano mkuu maalumu, kabla ya ule wa kawaida wa mwaka 2018 kwa mujibu wa Katiba, utafanyika pale chama hicho kitakapopata uwezo wa kifedha.
Akiandika katika mtandao wake wa Facebok, Mtatiro alisema, “Nimepokea majukumu niliyokabidhiwa na Baraza Kuu la chama changu. Siwezi kuepuka majukumu haya muhimu kwa wakati huu ambapo chama kinahitaji mchango wangu. Niko imara sana, natambua nimepewa majukumu wakati gani na nianze na mguu upi kwenda mbele”.