Jeshi
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata raia wawili wa
China kwa makosa ya utekaji nyara mfanyakazi wa kasino ya Le Grande
iliyopo maeneo ya Upanga, ambaye pia ni mchina aliyefahamika kwa jina la
Liu Hong (48).
Kamishna
wa Kanda hiyo, Kamanda Simon Sirro leo amewaambia waandishi wa habari
kuwa, wachina hao walimteka Hong na kumfanyia vitendo vya ukatili ambapo
walitoa masharti ya kupatiwa dola za kimarekani 19,000 ili wamuache
huru.
Kamanda
Sirro amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Wang Young Jing (37) na Chen
Chung Bao (35).Amesema watuhumiwa hao baada ya kufanyiwa upekuzi katika
chumba walichomficha Hong walikuta bomba la sindano, kamba za plastiki
ambavyo vinasadikika kutumika kumjeruhi raia huyo wa china.
Amesema baada ya askari polisi kufanikiwa kumuokoa Hong walimpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu.
Aidha,
Kamanda Sirro ametoa taadhari kwa wakazi wa Dar es Salaam kuwa makini
na raia wa kigeni waishio nchini kwa kuwa baadhi yao hushughulika na
uhalifu ikiwemo utekaji nyara.
Amewataka
wananchi kutoa taarifa pindi watakapobaini kuwa kuna raia wa kigeni
wanaonyanyasa wazawa na kufanya vitendo vya kihalifu.